Kwaherini, Nawapenda wote; Michael Jackson afariki dunia.
26 Juni 2009Mfalme wa muziki wa Pop kutoka Marekani Michael Jackson amefariki akiwa na umri wa miaka 50.Mwanamuziki huyo amefariki jana saa nane na dakika 26 saa za Los Angeles.Kifo cha Mwanamuziki huyo kimethibitishwa na mtaalamu wa matibabu katika mji huo ambaye amesema kwamba kimetokana na mshtuko wa moyo na alikuwa na matatizo ya kupumua hivyo basi maisha yake hayakuweza kuokolewa.Michael Jackson alikuwa amepangiwa kuwatumbuza maelfu ya mashabiki wake katika mlolongo wa matamasha mjini London mwezi Ujao.
Hivyo ndivyo alivyotaka kuikamilisha kazi yake ya muziki,,,kwa njia ya aina yake.Michael Jackson aliyejipa jina la mfalme wa muziki wa Pop alitaka kurudi tena jukwaani kuwatumbuiza mashabiki wake kwa mara ya mwisho licha ya uvumi kutoka kila pembe juu ya hali yake ya kiafya.Atakumbukwa daima,mnamo mwezi Marchi aliwaahidi mashabiki wake kuwapa tamasha la nguvu katika mlolongo wa burudani kwenye mji wa London.
'Hiyo itakuwa ni mara yangu ya mwisho kuonekana kwenye shoo mjini London.itakuwa hiyo tu,na nikisema, ''hiyo ndiyo itakuwa ya mwisho'', basi nafikiri ninamaana nitacheza nyimbo zote mashambiki wangu wanazotaka kuzisikia''
Nyimbo hizo ni zile za vibao vilivyotamba na kutia fora sana kutoka miaka ya themanini kama vile Billie Jean au Thriller.Albamu ya Michael Jackson ya Thriller kutoka mwaka 1982 ilipata umaarufu mkubwa sana na kufanikiwa katika kipindi kirefu ambapo iliuza takriban nakala millioni 65.Kwa jumla karibu albamu millioni 750 za Michael Jackson zimeuzwa kote duniani.Lakini kitakachokosa kusahaulika ni mtindo wake wa kipekee wa kucheza unaofahamika kama ''Moonwalk''
Kaka yake Jermaine akizungumzia juu ya kifo cha Michael amesema----
''Kakayangu,mfalme wa Pop Michael Jackson alifariki alhamisi saa nane na dakika 26 mchana.Inaaminika alipata mshtuko wa moyo nyumbani kwake.Allah awe pamoja nawe daima Michael''
Michael Joseph Jackson alianza taaluma ya muziki akiwa kijana mdogo wa shule.Mapema katika mwaka wa 1970 aliibuka na kundi moja likiwa linawajumuisha kakazake kundi lililojulikana kama The Jackson Five ambapo miongoni mwa vibao vilivyotia fora kutokana na kundi hilo ni pamoja na ABC na I'll be there yaani nitakuweko.
Chini ya usimamizi mkali wa babayao Joe Jackson watoto hao walifanikiwa kuwa wacheza shoo hodari na maarufu na Michael Jackson baadae alizungumzia matatizo aliyokumbana nayo utotoni....
Mashabiki kote ulimwenguni wameshtushwa na kifo cha mwanamuziki huyo nje ya kituo cha matibabu cha UCLA mjini Los Angeles mamia wamekusanyika wakiwa na hisia mbali mbali---
''Haiwezekani,siamini nasikitika sana alikuwa na kipaji na nitamkosa kwa hilo---
''Ntasema alikuwa machachari akisema watu waserebuke alitaka watu wafanye hivyo na aliweza kumfanya mtu atambue alikotoka na hiyo ndo sababu nampenda---
Katika kipindi chote cha kazi yake kama mwanamuziki Michael Jackson amepata tunzo zisizoweza kuhesabika ikiwa ni pamoja na 13 za kuwa mwanamuziki bora katika tunzo la Grammy nchini Marekani.Lakini mwanamuziki huyo hakugonga tu vyombo vya habari kutokana na kazi yake ya Muziki lakini pia kutokana na mabadiliko yaliyomtokea katika muonekano wake-Mabadiliko ya kutoka kuwa Mmarekani mweusi hadi kufikia kuwa kama mzungu akiwa na ngozi nyeupe na pua ndefu.Alikanusha lakini kwamba amefanyiwa opresheni ya kumbadilisha maumbile.
Mwaka 1993 aligonga pia vichwa vya habari kufuatia kashfa ya kuhusishwa na tuhuma za kumlawiti mtoto mdogo wa kiume hata hivyo nyota huyo wa muziki wa Pop aliepuka kesi hiyo lakini baada ya kutolewa dhamana ya dolla millioni moja.Mwaka 2005 akagonga tena vichwa vya habari akituhumiwa kuwalawiti watoto wadogo na mara hii kesi ilikuwa kubwa na kuchukua muda mrefu ambapo pia maisha yake ya siri yalianza kuwekwa hadharani----Baada ya kukutikana hana hatia Michael Jackson aliondoka Marekani na kwenda kuishi katika mojawapo ya nchi za kiarabu.Na kabla ya kifo chake alikuwa ameshajiandaa kurudi tena kwa kishindo katika ulimwengu wa Muziki ambapo alisema ni hatua yake ya mwisho ya kuuaga ulimwengu huo katika tamasha lililopewa jina Ni mara ya mwisho-----
Hii ni mara ya mwisho,ninaifunga pazia,tutaonana mwezi wa July.......
Hata hivyo ukipanga lako mungu ana lake,ahadi hiyo haitotimia badala yake mamilioni ya mashabiki wake kote duniani wanaendelea kushangazwa na taarifa za kifo cha mwanamuziki huyo aliyefariki akiwa na umri wa miaka 50.Michael Jackson aliwahi kuoa mara mbili-mke wake wa kwanza alikua Lisa Marie,mtoto wa mwimbaji maarufu Marehemu Elvis Presley. Michael Jackson ameacha watoto watatu.
Mungu ailaze roho yake mahala pema.
Mwandishi Henn Susanne/Saumu Mwasimba
Mhariri: Josephat Charo.