Kwanini New Caledonia imekumbwa na ghasia?
16 Mei 2024Kisiwa cha New Caledonia kinapatikana, Kusini mwa bahari ya Pasifiki, Mashariki mwa Australia na kiko chini ya himaya ya Ufaransa. Bunge la Ufaransa mjini Paris limekuwa likijadili muswaada wa kufanya mageuzi ya katiba ya kisiwa hicho ili kuwapa fursa raia wake wasiokuwa wenyeji wa kisiwa hicho kuwa na haki ya kupiga kura.
Lakini baadhi ya viongozi wa New-Caledonia wanakhofia muswaada huo utayavunja nguvu maamuzi ya wakaazi asilia wa kisiwa hicho kupitia michakato ya uchaguzi.Na mageuzi hayo ya sheria ya uchaguzi ndiyo mvutano wa hivi karibuni kabisa katika mapambano ya miongo kadhaa ya watu wa New Caledonia kuhusu dhima ya Ufaransa ndani ya kisiwa hicho.
Maandamano yaliyoshuhudiwayamezichochea mamlaka kufunga uwanja wake wa ndege wa kimataifa na kutangaza hatua ya kuzuia watu kutembea katika mji mkuu Noumea pamoja na kupelekwa kwa maafisa wa polisi kuweka usalama huku maduka na magari yakiteketezwa.
New Caledonia ni kisiwa ambacho kinapatikana kiasi kilomita 1,500 kutoka Mashariki mwa Australia na ni nyumbani kwa watu 270,000 ikijumuisha wakaazi asilia au wazawa wa kisiwa hicho asilimia 41 na wakaazi wenye asili ya barani Ulaya wapatao asilimia 24 wengi wakiwa ni Wafaransa.
Kisiwa hicho kiligunduliwa mwaka 1774 na Muingereza James Cook aliyekuwa akisafiri maeneo mbalimbali ya dunia kwa shughuli za uvumbuzi, lakini mwaka 1853 kilinyakuliwa na Ufaransa iliyokitumia kama eneo lake la kuwatenga wahalifu mpaka kuelekea karne ya 20. Lakini kwanini kisiwa hicho ni muhimu.
Soma:Ufaransa yapeleka wanajeshi New Caledonia kuzima ghasia
New Caledonia ni moja ya maeneo matano ya visiwa katika eneo hilo linalozunguukwa na bahari ya Hindi na Pasifik kinachodhibitiwa na Ufaransa na muhimu sana katika mpango wa rais Emanuel Macron wa kuimarisha ushawishi wake katika eneo hilo la Pasifik.
Pia ni wazalishaji nambari tatu wa madini ya Nickel duniani, lakini kisiwa hicho kadhalika kiko kwenye eneo la kimkakati katika siasa za kikanda linapohusika suala la mipaka ya bahari ambako China na Marekani zinavutana kupata nguvu na ushawishi kwenye masuala ya kiusalama na kibiashara. Rais Macron bila ya kuitaja China,aliwahi kusema kwamba hatua ya Ufaransa ya kutanua ushaishi wake katika ukanda huo ni kuhakikisha kuna maendeleo yanayozingatia sheria.
Historia ya Ufaransa ndani ya kisiwa hicho
Na kwahakika kuna historia ndefu kati ya kisiwa hicho na Ufaransa.New Caledonia kiliingia kwenye himaya ya Ufaransa mwaka 1949 na kuanzia miaka ya 1970 baada ya kugundulika rasilimali ya Nickel ambayo iliwavutia wageni wengi kuingia,ikazuka mivutano katika kisiwa hicho,ikishuhudiwa migogoro mbali mbali kati ya Ufaransa na wakaazi asilia wanaodai uhuru wa kisiwa hicho.
Soma: Macron aitisha kikao cha dharura kujadili ghasia kisiwa cha Caledonia
Mnamo mwaka 1998 yakapatikana makubaliano yaliyosaidia kuumaliza mgogoro ambapo chini ya makubaliano hayo mambo kadhaa yakuelekea kujitenga kwa kisiwa hicho hatua kwa hatua pamoja na kuwekwa sheria ya uchaguzi iliyotowa haki ya kupiga kura kwa wakaazi asilia tu na wakaazi waliohamia kwenye kisiwa hicho kabla ya mwaka 1998.
Na makubaliano hayo pia yalitowa nafasi ya kufanyika kura ya maoni mara tatu ya kuamua juu ya mustakabali wa kisiwa hicho.Na mara zote tatu za mchakato huo wa kura ya maoni, suala la kujitenga lilikataliwa.
Kura ya mwisho ya maoni ilifanyika mwaka 2021 na baada ya matokeo,rais Emmanuel Macron alisema Ufaransa inapendeza zaidi kwasababu New Caledonia imeamuwa kubakia kuwa sehemu ya nchi hiyo.
Lakini ni muhimu kutaja kwamba kura hiyo ya maoni ya mwaka 2021 ilisusiwa na vyama vyote vinavyounga mkono uhuru wa kisiwa hicho,kufuatia janga la Corona na kwahivyo bado yapo mashaka mengi kuhusu uhalali wa matokeo ya mchakato huo.
Mzizi mkubwa wa fitna ni sheria ya uchaguzi,chini ya makubaliano ya rasimu ya Noumea,chaguzi ndani ya kisiwa hicho zinapaswa kufanywa na wakaazi asilia na wale walioanza kuishi kwenye kisiwa hicho kabla ya 1998 tu na watoto wao.Ufaransa lakini inahisi utaratibu huo unaotumika sasa sio wa kidemokrasia na inataka watu wote walioishi katika kisiwa hicho kwa takriban miaka 10 pia wapate haki hiyo ya kupiga kura.
Ripoti: Macron atangaza hali ya hatari kisiwa cha New Caledonia
Baraza ya seneti la Ufaransa lilipitisha mapendekezo ya mageuzi ya katiba kwa misingi hiyo mnamo mwezi Aprili na sasa bunge linajadili muswaada huo na kura ya mwisho itakotowa uamuzi itapigwa Jumanne.