Le Pen apinga kupeleka wanajeshi wa Ufaransa nchini Ukraine
6 Julai 2024Katika mahojiano na kituo cha utangazaji cha kimarekani, CNN, Bi Le Pen amesema ikiwa chama chake cha National Rally (NR) kitapata kauli katika masuala ya uongozi wa nchi, hakitairuhusu Ukraine kutumia silaha za Ufaransa za masafa marefu katika vita vyake dhidi ya uvamizi wa Urusi.
Chama cha National Rally kilipata kura nyingi katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa bunge, ambao duru yake ya pili na ya mwisho inafanyika Jumapili.
Katika mazungumzo yake na CNN, Le Pen anayetarajiwa kuwa mgombea urais katika uchaguzi wa rais wa 2027 ameongeza kuwa serikali ya chama cha NR haitaruhusu kwa vyovyote vile wanajeshi wa Ufaransa kupelekwa katika ardhi ya Ukraine.
Soma zaidi:Chama cha Le Pen chashinda duru ya kwanza Ufaransa
Kwa kauli hiyo alikuwa akithibitisha msimamo wa chama chake, kuhusiana na matamshi ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa mapema mwaka huu, ambapo alikataa kuondoa uwezekano wa kuwapeleka wanajeshi wa Ufaransa nchini Ukraine kuwapa mafunzo wanajeshi wa nchi hiyo.
Hayo yakijiri, kiongozi wa sasa wa chama cha National Rally Jordan Bardella ambaye yumkini atakuwa waziri mkuu ikiwa chama chake kitapata ushindi katika duru ya pili ya uchaguzi wa bunge, amesema kuwa ingawa anaunga mkono haki ya Ukraine kulinda uhuru wake wa kieneo, amepinga Ufaransa kuipa nchi hiyo silaha za masafa marefu, akisema zinaweza kuzidisha mivutano.
-dpae