Lebanon yaanzisha uchunguzi kuhusu mkasa wa Beirut
5 Agosti 2020Akizungumza mapema katika hotuba iliyorushwa na televisheni wakati wa kuanza kikao cha Baraza la Mawaziri, rais Aoun amesema wamedhamiria kuchunguza na kufichua kile kilichotokea na kisha kuwaadhibu wale walihusika.
Uchunguzi wa awali umebaini kuwa uzembe wa miaka mingi wa kuhifadhi kemikali hatari katika ghala moja karibu na bandari mjini Beirut ndiyo chanzo cha mlipuko wa jana uliowauwa watu 100 na kujeruhi maelfu wengine.
Rais Aoun ameitumia hotuba yake kuendelea kutoa rai kwa mataifa mengine duniani kuisadia Lebanon katika juhudi zinazoendelea za kutafuta wahanga pamoja pia na kuzishukuru nchi ambazo tayari zimeahidi kutuma msaada.
"Ninawashukuru maafisa wote wa nchi jirani na rafiki waliowasiliana nasi kuonesha mshikamano na nia yao ya kutusaidia, ninawarai kuongeza kasi ya kuzisaidia hospitali zetu, familia zilizoathirika na kutusaidia kurekebisha uharibifu ulioyakumba majengo na bandari ya Beirut." amesema Auon.
Juhudi za uokozi zinaendelea
Siku nzima ya leo vikosi vya uokozi vimeendelea na juhudi za kuwatafuta watu waliokwama kutoka vifusi vya majengo yaliyoporomoka pamoja na kuanza matengenezo baada ya mlipuko wa jana kuharibu kwa sehemu kubwa majengo na mali nyingine.
Salamu za rambirambi na ahadi za msaada zimeendelea kumiminika kutoka kwa washirika wa karibu na hata mahasimu wa Lebanon kutokana na mkasa wa siku ya Jumanne.
Mataifa ya ghuba yamekuwa ya kwanza kutuma msaada baada ya Qatar kupakia shehena ya vitanda vya hospitali, majenereta na shuka inayotarajiwa kuwasili baadae leo mjini Beirut.
Umoja wa Ulaya, Uturuki na mataifa mengine mengi yametangaza kutuma msaada wa kitaalamu na kiutu kwenda Lebanon kusaidia juhudi za uokoaji.
Kansela Merkel atuma salamu za pole
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ambaye nchi yake pia imeahidi kuisaidia Lebanon ametuma salamu za pole kwa waziri mkuu Hassan Diab na kusema amefadhaishwa na mkasa uloikumba nchi hiyo.
Salamu za pole na rambi rambi zimetolewa pia na rais wa China Xi Jinping, Hassan Rouhani wa Iran, Donald Trump wa Marekani, Papa Francis na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guetteres.
Wakati huo huo rais Emmanuel Macron wa Ufaransa atakwenda nchini Lebanon kesho Alhamisi kwa ziara fupi ya kutoa pole na kuonesha mshikamano na taifa hilo la mashariki ya kati ambalo pia linakabiliwa na hali mbaya ya uchumi.
Ofisi ya rais Macron imesema kiongozi huyo atakutana na wenzake wa Lebanon na tayari Ufaransa inatuma maelfu ya tani za msaada na wafanyakazi wa uokozi kupiga jeki zoezi linaloendelea la kutafuta wahanga na kuwatibu majeruhi.
Mwandishi: Rashid Chilumba/DPA/AFP/REUTERS/AP
Mhariri: Gakuba, Daniel