Leo ni miaka 20 tokea Nelson Mandela atokea gerezani
11 Februari 2010Pale mzee Nelson Mandela alipotoka kwenye gereza la Victor-Vorster, siku kama leo ,Februari, 11,1990,miongoni mwa mashabiki walimuangalia alfu kadhaa wa kiafrika, walikuwa pia wazungu wa Afrika Kusini.
"Madiba" kama wanavyomuita mzee Mandela,akafaulu kufanya kile ambacho siasa zilishindwa nchini.Nacho ni kujenga daraja kati ya waafrika na wazungu.
Miaka 20 tangu kutoka korokoroni na miaka 16 tangu kuchaguliwa rais wa kwanza wa kiafrika nchini Afrika kusini,Mandela, anaendelea kuwa kama bado rais wa nchi hiyo.Akiwa kioo safi cha usadifu , mara nyingi mkosoaji,mzee Mandela amekuwa akisimamia maslahi ya kila upande miongoni mwa wananchi wake.
Leo miaka 20 tangu kutoka gerezani Bw.Mandela, kizazi kilichozaliwa baada ya mfumo wa ubaguzi na mtengano-aparthied- kina vuna matunda ya vita vya ukombozi alivyoongoza mzee Mandela.
Katiba ya Afrika Kusini, ni miongoni mwa zile huru duniani.Vyombo vya habari na jamii za kiraia ,ni huru na nchi hii imechanganya watu wa asili,jadi na makabila mbali mbali kuliko kwengineko kokote kule barani Afrika.
Mkumbo wa kuhama kwa wataalam ulionekana miaka ya 1990 pale baadhi ya wazungu walipoanza kufunga virago kuihama Afrika Kusini,sasa umesita.
katika miji kama Capetown,Durban na Johannesberg,tabaka ya waafirika ya kati na ile yenye pato inatamba.
Kwa jicho la tabaka la zamani la mabwanyenye majarabio ya kujenga jamii ya waafrika kusini wa rangi mbali mbali "Rainbow Nation", linaona hali ni vyengine kabisa. Kule ambako wazungu wasio na maskani wanaomba katika njia-panda, wanalalamika kuteremka kwa hali za maisha ,daraja za elimu na huduma za afya.Kuwatanguliza waafrika kushika nyadhifa fulani,wanadai, ni aina mpya ya mfumo wa ubaguzi na mtengano.Kumeongezeka pia uhalifu na rushua.
Muandishi habari wa gazeti la Handelsblatte nchini Afrika kusini,Wolfgang Drechsler,tangu miaka 25 sasa akijionea mabadiliko kwa macho yake kutoka dola la dhulma lililonyima haki na kuwa dola changa la kidemokrasi. Anasema:
" Ilikuwa nchi ambamo hali ya hatari iliselelea,anchi ambayo vikosi vya wauaji vikifanya kazi zao,nchi ambayo walio-wengi hawana haki.Sasa ukitupa macho na kuangalia kimtokea nini tangu enzi hizo ,unabidi kusema wazi:
Afrika kusini, imegeuka nchi bora ya kuishi.Bado ina matatizo mengi yanayoumiza kichwa, lakini, kama tujuavyo, imegeuka kuwa nchi ya kidemokrasi ambamo hivi sasa mamilioni ya wananchi wake alao wana matumaini ya maisha bora."
Kwa sherehe zinazofanyika leo ,anaonya Drechsler, hatahivyo, kushangiria tu kuwa kila kitu sawa si barabara.
Ana shaka shaka nyingi katika baadhi ya mabadiliko yaliyotokea. Ujeuri wa madaraka makuu wa chama-tawala cha ANC -chama chenye wingi mkubwa Bungeni.
Kiwango kikubwa cha rushwa na serikali ambayo imegeuzwa kama duka la kila mmoja kuzoa atakacho,Kuunga mkono yanayopita nchi jirani ya Zimbabwe na kutochukuliwa hatua barabara za kupiga vita Ukimwi.
Madhila yote hayo yamefanyika chini ya mzee Mandela na kwa bahati mbaya, kuna mengi yaliyokwenda kombo na hayafai kusahauliwa hata ikiwa kwa jumla, yafaa kuungama nchi hii, imepiga hatua za maendeleo.
Isipokuwa sasa inakaribia kuacha mkondo huo mwema ,yaani inafuata sasa ile njia ya kiafrika ya utawala wa chama kimoja,chini ya uongozi mmoja wenye mamlaka makuu.Na hii ni hali ambayo, tayari wakati wa mfuasi wa Mandela, rais Thabo Mbek, ilionekana.Na sasa hata imezidi chini ya uongozi wa rais wa sasa Jacob Zuma.
Afrika Kusini, sio tu nchini Ujerumani inafahamika kuwa ndilo gurudumu la uchumi na la kisiasa la bara la Afrika ambalo mchango wake katika utawala bora na katika biashara ya dunia hatahivyo, una kasoro.
Uwezo wa kiuchumi wa Afrika kusini, umebainika hasa katika vita vya kupambana na msukosuko wa fedha na wa kiuchumi ulimwenguni-amesema Bw.Michael Kleinert ,kiongozi wa Shirika la Ujerumani la kukuza biashara na Afrika Kusini:
Anasema kwamba, hata Afrika kusini, imeathrika na msukosuko wa kiuchumi,lakini wachambuzi ambao walidai hapo kabla kuwa itakumbwa na msiba mkubwa, msiba huo haukutokea.
Mwandishi: Ludger Schadomsky /DW-Amharic
Mtayarishi:Ramadhan Ali
Uhariri: Abdul-Rahman