1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Leverkusen yateleza dhidi ya Eintracht Frankfurt

16 Desemba 2013

Matumaini ya Bayer Leverkusen kutwaa taji la ligi msimu huu la Ligi Kuu ya Soka Ujerumani - Bundesliga yamepata pigo, baada ya kuduwazwa goli moja kwa sifuri na washika mkia Eintracht Frankfurt.

https://p.dw.com/p/1AaRh
Fußball Bundesliga 16. Spieltag Bayer 04 Leverkusen vs. Eintracht Frankfurt
Picha: Getty Images

Vijana hao wa kocha Sammi Hypia hata hivyo bado wako katika nafasi ya pili nyuma ya viongozi Bayern Munich ambao waliwashinda HAMBURG magoli matatu kwa moja. Bayern wako nchini Morocco kwa kinyang'anyiro cha Kombe la Dunia la Vilabu na watapambana kesho Jumanne na mabingwa wa bara Asia Guangzhou Evergrande FC katika nusu fainali kabla ya fainali ya Jumamosi.

Kwingineko, Schalke walifanikiwa kumwondolea shinikizo kocha Jens Keller kwa kusajili ushindi wa magoli mawili kwa sifuri dhidi ya Freiburg na kusonga hadi nafasi ya sita

Nao nambari tatu Borussia Dortmund walilazimika kutoka nyuma magoli mawili na kulazimisha sare ya mbili mbili na Hoffenheim, lakini ina maana wamedondosha pointi baada ya kushinda mchuano mmoja tu kati ya tano za mwisho. Sasa wako nyuma ya viongozi na pengo la pointi 12.

Borussia Moenchengladbach ilishindwa kutumia vyema matokeo ya mchuano wa Dortmund, kwa kutoka nao pia sare ya kutofungana goli na Mainz 05. bado wako katika nafasi ya nne kwenye ligi, wakiwa pointi sawa na Dortmund, 32.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman