1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu bila ya Messi na Ronaldo

18 Septemba 2023

Kwa mara ya kwanza msimu huu, Ligi ya Mabingwa barani Ulaya itayakosa majina makubwa kwenye ulimwengu wa soka kama vile Cristiano Ronaldo na Lionel Messi.

https://p.dw.com/p/4WUEC
Wachezaji nyota Lionel Messi na Cristiano Ronaldo
Wachezaji nyota Lionel Messi na Cristiano RonaldoPicha: Franck Fife/AFP

Cristiano Ronaldo alikuwa wa kwanza kutimkia Ligi Kuu ya Saudi Arabia ambapo sasa anaichezea klabu ya Al Nassr huku Lionel Messi akicheza soka lake la kulipwa na klabu ya Marekani ya Inter Miami.

Wachezaji wengine ambao pia hawatoshiriki Ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu huu ni mshambuliaji wa timu ya taifa ya Brazil Neymar, mshambuliaji raia wa Ufaransa Karim Benzema. Wawili hao wamejiunga na Al Hilal na Al Ittihad mtawalia.

Winga wa timu ya taifa ya Senegal Sadio Mane pia amejiunga na klabu ya Al Nassr akitokea Bayern Munich.

Macho yote msimu huu yanawatazama nyota wa Paris St Germain Kylian Mbappe na mfungaji hodari wa Manchester City Erling Haaland.

Kadhalika, mashabiki pia wana shauku ya kutazama kipaji cha kinda wa Barcelona Lamile Yamal. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 16 ameingia kwenye rekodi kwa kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kuichezea Barcelona na timu ya taifa ya Uhispania.