1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lissu awawekea pingamizi Magufuli, Lipumba

26 Agosti 2020

Mgombea urais kupitia chama cha upinzani cha CHADEMA nchini Tanzania anasema amemwekea pingamizi Rais John Magufuli anayetetea nafasi hiyo kupitia chama tawala, CCM, na Ibrahim Lipumba wa chama cha upinzani cha CUF.

https://p.dw.com/p/3hXw3
Tansania Dar es Salaam | Politiker | Tundu Lissu
Picha: DW/S. Khamis

Kupitia akaunti yake Twitter, Tundu Lissu, aliandika kwamba hadi kufikia saa 10:05 alasiri alipokuwa akiondoka kwenye ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) mjini Dodoma hakukuwa na pingamizi lolote lililowekwa dhidi yake, badala yake ni yeye aliyekuwa amewawekea pingamizi hilo wagombea urais wa CCM na CUF.

"Ninaondoka kwenye ofisi ya NEC baada ya kuwasilisha mapingamizi dhidi ya uteuzi wa John Pombe Magufuli wa CCM na Prof. Ibrahim Lipumba wa CUF kwa uvunjaji mkubwa wa sheria za uchaguzi. Kufikia saa 10:05 majira ya hapa, hakukuwa na mapingamizi yoyote dhidi yangu. Pingamizi lolote la baada ya hapo litakuwa limepitwa na wakati," aliandika Lissu, ambaye kitaaluma ni mwanasheria.

Haikufahamika mara moja endapo NEC imeyafanyia kazi mapendekezo hayo na ikiwa Magufuli na Lipumba waliarifiwa kujibu kama ulivyo muongozo wa uchaguzi katika taifa hilo la Afrika Mashariki.

Hatua hii ya Lissu ilizuwa maswali mengi kwenye mitandao ya kijamii, ambapo wengine walisema ni njia ya kujilinda dhidi ya hatua kama hiyo kuchukuliwa kwake kama ambavyo ilikuwa ikihofiwa awali. 

NEC yaonya dhidi ya wagombea wanaojitangazia ushindi

Katika hatua nyengine, Tume hiyo ya uchaguzi ya Tanzania iliwaonya vikali wagombea waliojitangaza kushinda nafasi zao kwa kupita bila kupingwa kwenye nafasi za ubunge na udiwani.

Tansania Dodoma | Wahlkampf | CCM Partei
Mgombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, John Magufuli (kulia) na mgombea mwenza, Samia Suluhu Hassan.Picha: DW/S. Khamis

Kauli ya NEC ilifuatia kusambaa kwa taarifa nyingi zilizodai kwamba zaidi ya wagombea 15 wa chama tawala, CCM, walikuwa wamepita bila kupingwa baada ya waliokuwa wapinzani wao kuondolewa kwenye kiyang’anyiro hicho na wasimamizi wa uchaguzi kwa sababu mbalimbali.

Akitoa onyo hilo, Mkurugenzi wa tume hiyo, Charles Mahera, alisema "mamlaka ya kutangaza nani ameshinda na yupi ameanguka iko mikononi mwa tume, na siyo chombo kingine."

Vyombo vya habari ambavyo vilitajwa kuwa mshirika muhimu wa uchaguzi mkuu navyo vilinyooshewa kidole cha onyo vikitakiwa kutokuwa na haraka ya kutangaza mambo ambayo hayana ridhaa na tume hiyo.

Wakati tume hiyo ikiwaweka mguu sawa waandishi wa habari pamoja na baadhi ya wagombea, vyama vinavyoshiriki uchaguzi huo ambavyo vilidai kutoridhishwa na hatua za awali kutokana na wagombea wao kuenguliwa, vilikuwa vikiendelea na mchakato wa kukata rufaa.

Vyama hivyo vilidai kwamba asilimia kubwa ya wagombea wake wa ubunge na udiwani waliondolewa kwenye kinyang’anyiro hicho kwa njia ya mizengwe kwa ajili ya kutoa nafasi kwa upande wa pili wa kisiasa.

Chama cha ACT Wazalendo ambao nacho pia kimesimamisha wagombea wake katika maeneo mbalimbali ya nchi, kiliishutumu hatua ya kunyimwa fursa ya kugombea kwa wateule wake huku kikitoa taarifa ya kulaani vikali mwenendo huo.

Meneja kampeni wa chama hicho, Emmanuel Semvula alisema tayari chama hicho kilishawasilisha hoja zake NEC.

Ripoti ya George Njogopa/DW Dar es Salaam