Liz Truss waziri mkuu mpya Uingereza
5 Septemba 2022Truss, mwenye umri wa miaka 47, amemshinda waziri wa zamani wa fedha, Rishi Sunak, kwenye uchaguzi wa chama ambao ni wanachama hai 170,000 tu wa chama cha Conservative walioruhusiwa kupiga kura. Truss amepata kura 81,326 huku Sunak akipata 60,399.
Kwenye hotuba ya kushukuru kuchaguliwa kwake, waziri mkuu huyo mteule aliwaambia wajumbe wa chama chake kwamba anaamini atatimiza majukumu yake kikamilifu.
"Nawashukuru kwa kuniamini kuongoza chama hiki kikubwa kabisa cha kisiasa uliwenguni. Nitatekeleza mpango madhubuti kabisa wa kupunguza kodi na kuukuza uchumi wetu. Nitashughulikia suala la bei ya nishati, na pia masuala ya muda mrefu ya usambazaji wa nishati. Nitatimiza pia ahadi yetu kwenye huduma ya afya ya taifa, na tutayatimiza haya sote kwa pamoja kwa ajili ya nchi yetu." Alisema.
"Sasa ni muda wa kuungana na waziri mkuu mpya, Liz Truss, wakati akiiongoza nchi yetu kupitia kipindi kigumu." Aliandika Sunak kwenye ukurasa wake wa Twitter mara baada ya matokeo hayo kutangazwa.
Kwa upande wake, waziri mkuu anayeondoka, Borris Johnson, alikitolea wito chama tawala cha Conservative kushikamana, akisema anaunga mkono mipango ya Liz Truss ya kukabiliana na tatizo la hali ngumu ya maisha na kushughulia suala la ukosefu wa usawa.
Ulaya yakaribisha uteuzi wa Truss
Kwa upande wake, Rais wa Kamisheni ya Ulaya, Ursula von der Leyen, alisema anatazamia chini ya Liz Truss, Uingereza ingeliheshimu vifungu vyote vya mkataba wa Brexit.
"Tunakabiliana na changamoto nyingi pamoja, kutoka mabadiliko ya tabianchi hadi uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Natazamia mahusiano yenye maana, yanayoheshimu kikamilifu makubaliano yetu." Aliandika kupitia Twitter.
Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani amempingeza Liz Truss kwa ushindi wake, akimuhakikishia kuwa nchi hizo mbili zitaendelea kufanya kazi pamoja kama washirika na kama marafiki.
Kibaruwa kigumu
Truss anakabiliwa na kibarua kigumu cha kutekeleza ahadi zake za kupunguza makali ya maisha, wakati kila ishara ikionesha kuwa Uingereza inaelekea kwenye mserereko mkubwa wa kiuchumi.
Malkia Elizabeth II alitazamiwa kumteuwa rasmi Truss kuwa waziri mkuu mpya wa Uingereza siku ya Jumanne (Septemba 9) katika kasri ya Balmoral, Scotland.
Kampeni ya miezi miwili ya kuwania uongozi kati ya Truss na Rishi Sunak uliiwacha nchi kwenye ombwe la madaraka wakati ghadhabu za umma zikipanda kutokana na ugumu wa maisha na bei za vyakula na nishati.
Tangu atangaze kuondoka madarakani tarehe 7 Julai, Johnson hakuwa amefanya maamuzi yoyote makubwa ya kisera, huku maafisa wake wakisema kuwa hatua za kushughulikia mzozo wa bei ya nishati na gharama za maisha ingechukuliwa na serikali ijayo.