LRA kukutana na Museveni Alhamisi
31 Oktoba 2007Matangazo
Kundi la waasi wa kaskazini mwa Uganda la Lords Resistance Army LRA limesema litakuwa na mkutano huo wa aina yake pamoja na rais Yoweri Museveni mjini Kampala kesho alhamisi.
Mkutano huo utafanyika baada ya rais Museveni kurejea kutoka Marekani ambako alikutana na rais Gorge Bush na kuzungumzia kuhusu suala la amani kaskazini mwa Uganda.
Mkutano wa kesho utahudhuriwa na wajumbe wa ngazi ya juu ya kundi la LRA akiwemo mpatanishi mkuu wa kundi hilo Martin Ojul ambao watafika kwa mara ya kwanza mjini Kampala tangu kuanza kwa uasi kaskazini mwa nchi hiyo miaka 21 iliyopita ambapo maelfu ya watu waliuwawa na mamilioni ya wengine kuachwa bila makazi.Hata hivyo Joseph Kony kiongozi wa Kundi hilo hatahudhuria mkutano huo.