Lukashenko kufanya mazungumzo na Merkel juu ya uhamiaji
16 Novemba 2021Lukashenko amesema baada ya mazungumzo yake ya kwanza kwa njia ya simu jana Jumatatu na Merkel, Kansela huyo wa Ujerumani alijadiliana na viongozi wengine wa Umoja wa Ulaya kuhusu pendekezo la Belarus la kulitafutia ufumbuzi suala hilo la uhamiaji.
Rais huyo wa Belarus ameongeza kuwa anataka kuzuia malumbano zaidi juu ya mzozo wa wahamiaji kwenye mpaka wa nchi yake na Poland baada ya Umoja wa Ulaya kumshtumu kwa kuruhusu kimakusudi wahamiaji hao kuingia ndani ya mataifa ya Umoja wa Ulaya.
Soma pia: Ujerumani yautaka Umoja wa Ulaya kuzuia wahamiaji haramu wanaoingia Poland
Kwa mujibu wa shirika la habari la serikali la Belta, Lukashenko aliuambia mkutano wa baraza lake la mawaziri,"Hatuwezi kuruhusu suala hili kusababisha malumbano. Jambo la msingi kwa sasa ni kuilinda nchi yetu na kutoruhusu mapigano."
Juhudi za kidiplomasia za kuutatua mzozo huo wa wahamiaji zilishika kasi jana Jumatatu wakati Kansela Angela Merkel na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron walipoingilia kati kwa kujaribu kutumia ushawishi wao ili kuutatua mzozo huo ambao umesababisha maelfu ya wahamiaji kukwama kwenye mpaka wa Belarus na Poland chini ya baridi kali.
Abdullahi Najih, ni mmoja wa wakimbizi waliokwama kwenye mpaka wa Belarus na Poland.
"Umoja wa Ulaya unajaribu kadri ya uwezo wake kutatua matatizo yetu na kuturuhusu kuvuka mpaka na kuingia. Wanaishinikiza serikali ya Poland kufungua mpaka wake na kuturuhusu kuingia."
EU unamshtumu Lukashenko kwa kuwaruhusu wahamiaji kuvuka mpaka na kuingia Poland
Shirika la habari la serikali ya Belarus limeripoti kuwa Merkel alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na Lukashenko yaliyodumu kwa takriban dakika 50, likisema mazungumzo yao yalijikita katika kutuliza hali na kuwapa misaada ya kibinadamu wahamiaji. Hata hivyo, hakukuwa na tamko lolote kutoka upande wa Ujerumani kuhusu mazungumzo hayo.
Wakati huo huo, Rais Macron pia alifanya mazungumzo na Rais Vladimir Putin wa Urusi, ambaye ni mshirika wa karibu wa kiongozi huo wa Belarus.
Soma pia: Ulaya kuiwekea Belarus vikwazo vikali zaidi
Viongozi hao wawili walizungumzia juu ya jukumu ambalo Urusi inaweza kuchukua ili kuutatua mzozo huo. Kwa mujibu wa Kremlin, Putin amesema viongozi wa mataifa ya Umoja wa Ulaya EU wanapaswa kujadiliana moja kwa moja na Lukashenko juu ya mzozo huo.
Umoja wa Ulaya unaushtumu utawala wa Lukashenko kwa kuwaruhusu wahamiaji kimakusudi kuvuka mpaka na kuingia Poland, ikiwa kama njia ya kulipiza kisasi baada ya Umoja huo kukataa kutambua ushindi wake katika uchaguzi mkuu wa mwaka uliopita pamoja na kuiwekea vikwazo Belarus. Hata hivyo Lukashenko amekanusha madai hayo.