Lula asema BRICS inafanya juhudi kumaliza vita Ukraine
23 Agosti 2023Rais wa Brazil Luis Inacio Lula da Silva amesema leo kuwa nchi za kundi la BRICS zinashirikiana na Ukraine na Urusi katika juhudi za kumaliza vita. Lula amekosoa vikwazo vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika kuushughulikia mzozo huo.
Akizungumza katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Nchi zinazoinukia kiuchumi duniani - BRICS mjini Johannesburg, Lula amesema idadi inayoongezeka ya nchi, miongoni mwao wanachama wa BRICS, zinashiriki katika mawasiliano ya moja kwa moja na Moscow na Kyiev.
Naye Rais Vladimir Putin wa Urusi amewaalika viongozi wenzake wa BRICS, kufanya mkutano wa kilele ujao nchini mwake, huku mwenyewe akishindwa kusafiri kwenda Afrika Kusini kwa mkutano wa mwaka huu, kutokana na kuwepo hati ya kumkamata iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC.
Putin aliwakilishwa na waziri wake wa mambo ya nje Sergei Lavrov, na yeye mwenyewe akashiriki kupitia video.