Luxembourg. Mawaziri kuishawishi Austria kukubali kuijadili Uturuki.
3 Oktoba 2005Mawaziri wa mambo ya kigeni wa umoja wa Ulaya wanakutana mjini Luxembourg kujaribu kuishawishi Austria kuachana na upinzani wake kwa Uturuki kuwa mwanachama kamili wa umoja huo, katika kikao cha dharura kabla ya umoja huo kuanza mjadala juu ya Uturuki kuwa mwanachama.
Majadiliano ya uanachama na Uturuki yamepangwa kuanza siku ya Jumatatu, lakini Austria imepinga katika dakika za mwisho kuanza rasmi mazungumzo hayo na taifa hilo ambalo lina Waislamu wengi na badala yake nchi hiyo imependekeza kuwa Uturuki ipewe nafasi ya kuwa mshirika mpendelewa.
Uturuki imesema kuwa haitakubali chochote zaidi ya kujadiliwa kuwa mwanachama wa umoja wa Ulaya.
Waziri mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema kuwa viongozi wa Ulaya ni lazima waamue iwapo umoja wa Ulaya ufikie katika changamoto ya kuwa nguvu kuu ya dunia ama ibaki kuwa Club ya Wakristo tu.