Maadhimisho ya miaka 70 ya uhuru India
15 Agosti 2016Sherehe hizi zimefanyika siku moja baada ya Pakistan kusherehekea siku ya uhuru wake na rais wa nchi hiyo, Manmoon Hussain, kuzungumzia kuhusu eneo la Kashmir, ambalo linatawaliwa na India .
India husherehekea siku ya uhuru wake tarehe15 mwezi Agosti siku moja baada ya Pakistan. Zote mbili, India na Pakistan, zilipata uhuru wao kutoka Uingereza mwaka 1947 kama mataifa mawili tofauti, ingawa yalitawaliwa kama taifa moja kubwa, siku hizo ikiitwa Bara Hindi.
Mataifa hayo jirani yana historia ya uhusiano wa utata ambao mara nyingi kila mmoja humshutumu mwenzake kwa kuunga mkono harakati za upinzani, uhalifu na hata ugaidi katika maeneo yao.
Katika hotuba hiyo ya miaka 70 ya uhuru wa India, Waziri Mkuu Modi aliwalenga wale aliowaita "wafuasi wa ugaidi" na kuishtumu Pakistan huku akiepuka kutaja moja kwa moja mzozo uliodumu kwa mwezi mmoja sasa katika jimbo la Kashmir, ambalo linapigania kujitenga kwa miaka kadhaa, takribani tangu uhuru.
Baina ya Baluchistan ya Pakistan na Kashmir ya India
Mkoa wa Baluchistan umekuwa na misukosuko katika miaka ya hivi karibuni huku eneo la Kashmir nchini India likikabiliwa na mauaji ya takriban raia 50 wakati wa maandamano ya ghasia tangu mwezi Julai.
Katika hatua isiyokuwa ya kawaida wakati wa hotuba za siku ya uhuru nchini India, Waziri Mkuu Modi alizungumzia ngome za nchi nyingine kwa kutaja maeneo ya Baluchistan, Gilgit, Balistan na eneo la Kashmir linalomilikiwa na Pakistan na kusema kuwa ulimwengu unatazama na kwamba watu wa Baluchistan, Gilgit na eneo la Kashmir linalomilikiwa na Pakistan wamemshukuru sana katika siku chache zilizopita.
Wakati Modi alipokuwa akizungumza, washambuliaji walivamia kituo kimoja cha polisi katika eneo la Srinagar huko Kashmir na kumuuwa afisa mmoja wa polisi na kuwajeruhi wengine 10. Wanamgambo wawili waliuawa wakati wa tukio hilo.
Mataifa yote ya India na Pakistan yanamiliki maeneo ya Kashmir lakini kila moja linadai kumiliki jimbo hilo kikamilifu. Mataifa hayo mawili yamehusika katika vita mara mbili tangu kujinyakulia uhuru kuhusiana na eneo hilo lililo na waislamu wengi zaidi.
Siku ya Ijumaa Modi alikutana na viongozi wa kitaifa wa chama chake kuangazia njia za kumaliza mzozo wa Kashmir ulioanza mwaka 2010.
Hatua za ufanisi
Mbali na hayo, Modi pia alielezea maono ya umoja wa kitaifa na maendeleo katika hotuba yake ya tatu ya mwaka katika eneo la Red Fort huko Old Delhi ambayo katika muda wa dakika 94, ndio iliyokuwa hotuba ndefu zaidi kuwahi kutolewa na kiongozi huyo wa umri wa miaka 65.
Ikilinganishwa na hotuba nyingine, Modi alitoa ripoti kuhusu juhudi za kuimarisha maisha ya wananchi wa kawaida nchini India akielezea bayana ufanisi katika miradi ya kusambaza umeme katika maeneo ya mashambani, ujumuishaji katika maswala ya fedha na utoaji huduma za afya.
Aliunga mkono vita dhidi ya kupanda kwa gharama ya maisha na kuidhinisha lengo la asilimia 4 kwa makubaliano na gavana wa benki kuu, Raghuram Rajan.
Pia aligusia ufanisi wa marekebisho wa hivi punde wa serikali yake ambao ni kupitishwa kwa marekebisho yanayowezesha kuanzishwa kwa utozaji ushuru wa bidhaa na huduma mwaka ujao.
Alisema ni kupitia hatua hiyo ndipo uchumi utaweza kuimarika na akavishukuru vyama vya upinzani kwa kukubali kupitisha marekebisho hayo.
Lakini licha ya kampeni kabambe ya Modi iliyomwezesha kupata ushindi mkubwa mnamo mwaka 2014 ambao haujawahi kushuhudiwa katika muda wa miongo mitatu iliyopita, hajafikia upeo wa matamshi ya aliyekuwa waziri mkuu wa kwanza wa nchi hiyo, Jawaharlal Nehru.
Mwandishi: Tatu Karema/dpa/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef