Maafisa wa fedha duniani kuchukua hatua za kuukuza uchumi
10 Oktoba 2014Mawaziri wa fedha na magavana wa benki kuu za kundi la nchi ishirini zenye nguvu zaidi kiuchumi duniani ambazo ni pamoja na miamba wa uchumi wa tangu jadi Marekani, Ujerumani na Japan pamoja na nchi zinazoinukia kwa kasi kiuchumi kama Urusi na China wanakamilisha misururu ya mazungumzo ya siku mbili hii leo mjini Washington, Marekani huku wakitoa taarifa ya pamoja kuhusu malengo na kutarajiwa kuhutubia wanahabari baadaye leo.
Mikutano hiyo inakuja wakati kuna taarifa kutoka barani Ulaya kuwa hali ya kiuchumi ya nchi wanachama kumi na nane zinazotumia sarafu ya euro sio ya kutia moyo na huenda kuna hatari ya kushuhudia msukosuko mwingine wa kiuchumi katika kanda hiyo.
Ujerumani yapata hasara
Ujerumani hapo jana iliripoti mauzo yake ya nje yameshuhudia anguko kubwa zaidi katika kipindi cha miaka mitano mwezi Agosti, kufuatia kupungua kwa kiasi kikubwa cha mahitaji kutoka kwa washirika muhimu wa kibiashara wa taifa hilo katika kanda ya sarafu ya euro.
Australia ambayo ni mwenyeji wa mkutano wa kundi la nchi ishirini zenye nguvu zaidi za kiuchumi duniani mwaka huu inataka kupitishwa kwa mpango makhususi wa kuchukuliwa hatua ambazo zitaweka malengo ya kuuchochea uchumi wa dunia kwa angalau asilimia mbili katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Makadirio hayo ya ukuaji yanamaanisha kutahitajika kuongezeka kwa uzalishaji wa kiviwanda wa kiasi cha dola trilioni mbili ili kuliafikia lengo hilo katika kipindi hicho cha miaka mitano ijayo.
Baada ya kuidhinishwa na maafisa wakuu wa fedha, mpango huo wa kufufua uchumi utawasilishwa kwa Rais wa Marekani Barack Obama na viongozi wengine wa nchi za G 20 kutiwa saini katika mkutano wa kilele unaotarajiwa katikati ya mwezi ujao mjini Brisbane, Australia.
Vitisho kadha wa kadha vikwazo
Maafisa wa kiuchumi wamesema kuongeza matumizi ya fedha kwa ajili ya barabara, viwanja vya ndege an miundo mbinu mingine hakutatosha kuuinua uchumi wa dunia hadi kiwango thabiti hasa kutokana na kuongezeka kwa vitisho dhidi ya ukuaji wa uchumi kutoka kanda mbalimbali duniani.
Uchumi wa dunia unakabiliwa na vitisho mbali mbali vikiwemo mzozo wa Ukraine, kitisho cha kuongezeka kwa uasi unaoenezwa na makundi ya wanamgambo wenye itikadi kali kama linalojiita dola la kiislamu IS nchini Iraq na Syria na kuzuka kwa ugonjwa wa Ebola magharibi mwa Afrika.
Majadiliano hayo ya G20 yanafanywa kabla ya mikutano ya kila mwaka ya nchi wanachama 188 wa shirika la fedha duniani IMF na benki ya dunia.
Mwandishi:Caro Robi/ap
Mhariri:Josephat Charo