Khamenei aongoza ibada za kuaga miili ya Raisi na maafisa
22 Mei 2024Khamenei ameongoza shughuli hiyo iliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Tehran.
Vilio na maombolezo vikisikika kutoka kwa waombolezaji waliokusanyika kwa ajili ya kuwaaga viongozi wao. Majeneza yao yaliyokuwa yamezungushiwa bendera ya Iran, yalipangwa mbele ya maafisa wandamizi na mamia kwa maelfu ya waombolezaji.
Khamenei aliongozwa ibada ya kawaida tu ya kuswalia maiti, akitumia lugha ya Kiarabu kama ilivyoandikwa kwenye kitabu kitakatifu cha Kiislamu cha Quran. Mara baada ya sala Khamenei aliondoka.
Rais wa mpito wa Iran Mohammad Mokhber aliyekuwa amesimama karibu na Khamenei alionekana akibubujikwa machozi wakati ibada hiyo ikiendelea.
Soma pia: Heshima za mwisho kwa Ebrahim Raisi zaanza kutolewa Iran
Baadaye, waombolezaji waliyabeba majeneza hayo mabegani huku wakipaza sauti "kifo kwa Marekani," kisha wakayaweka kwenye lori lililokuwa wazi tayari kuanza kutembezwa kwenye mitaa ya mji mkuu Tehran hadi Azadi ama Bustani ya Uhuru eneo ambako Raisi alikuwa akilitumia kuhutubia.
Miongoni mwa waliohudhuria ni maafisa waandamizi wa Kikosi cha Walinzi wa Kimapinduzi, chenye ushawishi mkubwa nchini humo. Ismail Haniyeh, kiongozi wa wanamgambo wa Hamas wa Palestina pia alikuwepo. Ikumbukwe kundi hili linasaidiwa na Iran kijeshi katika vita vyake vinavyoendelea dhidi ya Israel katika Ukanda wa Gaza.
Inasemekana maafisa wa ngazi za juu zaidi ya 40 kutoka mataifa ya kigeni watakuwepo mjini Tehran kwa ajili ya mazishi hayo.
Soma pia: Scholz atuma risala za rambirambi kwa Iran
Mwili wake hatimaye utasafirishwa hadi katika mji mtakatifu kwa waislamu wa madhehebu ya Shia wa Qom. Kutoka hapo, utarejeshwa kwenye mji mkuu Tehran na kuwekwa kwenye Msikiti Mkuu wa Mosalla kabla ya kupelekwa nyumbani kwake huko Mashahd, mashariki mwa Iran kwa mazishi kesho Alhamisi.
Kifo chake kinatokea wakati kukishuhudiwa mgawanyiko mkubwa kati ya uongozi wa kidini na kwa kiasi kikubwa jamii ya Iran, kuhusiana na udhibiti mkali wa masuala ya kijamii na kiuchumi na kusababisha hali kuwa ngumu.
Soma pia: Iran kufanya uchaguzi mkuu wa rais mnamo Juni 28
Rais Ebrahim Raisi, Waziri wa Mambo ya Nje Hossein Amirabdollahian na maafisa wengine walikuwa wakirejea Iran, wakitoka kuzindua bwawa lililoko kwenye mpaka kati ya Iran na Arzebaijan siku ya Jumapili wakati helikopta yao ilipoanguka kwenye maeneo ya milima iliyopo mkoa wa Varzaghan.