Maambukizi ya COVID-19 bado yaongezeka duniani
22 Juni 2020Wakati huo huo mataifa ya Ulaya yanafurhia ulegezwaji wa taratibu wa hatua za kuwazuwia watu kusalia majumbani mwao lakini katika mahospitali mataifa hayo yanajitayarisha kwa wimbi la pili la maambukizi.
Idadi ya maambukizi nchini India imepanda kwa karibu watu 15,000 hadi hii leo Jumatatu na kufikia kesi 425,282, ambapo watu zaidi ya 13,000 wamefariki, wizara ya afya imeripoti.
Baada ya kulegeza hatua za kuwazuwia watu kusalia majumbani mwao, serikali ya India imetumia treni maalum kuwarejesha maelfu ya wafanyakazi wahamiaji kwenda katika vijiji vyao katika wiki za hivi karibuni.
Karibu asilimia 90 ya wilaya masikini nchini India zina kesi za maambukizi, licha ya kuwa maambukizi zaidi yanabakia kuwa Delhi, Maharashtra, na Tamil Nadu, majimbo ambayo yana miji mikubwa. Maambukizi yamepungua nchini China na Korea kusini, ikionesha hatua za maendeleo katika kudhibiti mripuko mpya. Lakini licha ya hatua hizo katika kudhibiti virusi hivyo katika kanda ambazo ziliathirika mapema kutokana na kuzuka kwa virusi hivyo, dunani kwa jumla idadi ya kesi za maambukizi mapya imepanda katika siku za hivi karibuni.
Mahospitali yanapata shinikizo kuwahudumia wagonjwa
Nchini Brazil, Iraq, India na Marekani, mahospitali yamefikia katika hatua ya kushindwa kuwahudumia wagonjwa.
Karibu watu milioni 9 wameambukizwa na virusi vya corona na zaidi ya watu 468,000 wamefariki, kwa mujibu wa idadi iliyowekwa pamoja na chuo kikuu cha Johns Hopkins. Wataalamu wanasema idadi halisi ni ya juu zaidi, kutokana na ukomo wa kufanya uchunguzi pamoja na kile kinachofikiriwa kuwa ni idadi kubwa ya watu ambao hawaoneshi dalili.
Idadi ya kesi zilizothibitishwa nchini Ujerumani imepanda kwa watu 537 hadi watu 190,359, ikiwa ni data kutoka taasisi ya Robert Koch ya kudhibiti magonjwa ya maambukizi zimeonesha leo Jumatatu.
Idadi ya watu waliofariki imeongezeka kwa watu watatu, na kufikia watu 8,885.
Idadi ya kesi zilizothibitishwa katika machinjio nchini Ujerumani imepanda kwa watu 300 jana, hadi watu 1,331, wakati maafisa kutoka katika jimbo la North Rhine Westfalia wakifanya ziara katika eneo hilo ambalo limezusha hofu ya wimbi la pili la maambukizi. Maafisa walikuwa wanasubiri matokeo ya uchunguzi wa kiasi ya watu 250 kutoka idadi ya watu 6,139 ambao umekwisha fanyika katika kampuni hiyo ya machinjio.
Italia imeripoti vifo vipya 24 kutokana na ugonjwa wa COVID-19 jana, ikiwa ni kiwango cha chini cha vifo vya kila tangu Machi 2, mnamo wakati vifo vya watu 18 viliripotiwa.