Maandamano Bukavu kumtaka Rais Tshisekedi kuheshimu katiba
4 Agosti 2020Maandamano hayo yalianzia Place Mulamba hadi kwenye ofisi ya gavana wa mkoa wa Kivu kusini eneo la Nyamoma ambako walimkabidhi madai yao.
Pamoja na kutangaza kwamba wanaunga mkono taasisi zote za Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, wafuasi wa FCC wametaka uongozi wasasa kutekeleza majukumu yake kwa kufuata katiba ya nchi.
Wametoa pia onyo kwa Rais Félix Tshisekedi kutojaribu kuahirisha uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mnamo 2023.
Kwa zaidi ya mwezi mmoja, mtafaruku mkubwa umeibuka kati ya wanasiasa wa vyama vya FCC na vile vya CACH vinavyounga mkono rais wa sasa Félix Tshisekedi.
Maoni yakiwa yanatofautiana kuhusu masuala kadhaa ikiwemo mapendekezo ya mageuzi ya wabunge wa FCC ya sheria kuhusu idara ya mahakama.
Mapendekezo hayo yalipingwa vikali na muungano wa CASH, kiongozi mpya wa tume ya uchaguzi CENI Ronsard Malonda aliyekataliwa na CASH pamoja na upinzani wa Lamuka. Msuko-suko huo wa kisiasa ulichangia pia katika kufanyika kwa maandamano hayo.
Waandamanaji wengine walichukua fursa hii kulalamikia hali ngumu ya maisha wanayopitia, kutokana na viwango vya ubadilishaji wa sarafu ya dola ambavyo wakati huu vinayumba nchini Congo.
Gavana wa mkoa wa Kivu kusini Théo Ngwabidje amepokea barua ya madai hayo na ameahidi kuyafikisha kwa rais Félix Tshisekedi mjini Kinshasa.