1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano Misri baada ya uamuzi wa Mahakama

Mjahida 30 Novemba 2014

Mahakama Misri imetupilia mbali mashitaka ya mauaji dhidi ya rais wa zamani Hosni Mubarak, na kuwakasirisha wanaharakati ambao walihamasisha vuguvugu la maandamano ya umma yaliofikisha mwisho utawala wake mwaka 2011.

https://p.dw.com/p/1DxBZ
Baadhi ya raia wa Misri waandamana baada ya uamuzi wa Mahakama
Baadhi ya raia wa Misri waandamana baada ya uamuzi wa MahakamaPicha: picture-alliance/dpa/I. Farouk

Mashitaka hayo yalihusishwa na mauaji ya waandamanaji 800 katika maandamano ya kutaka mageuzi. Mahakama hiyo ya uhalifu mjini Cairo ilimfutia mashitaka pia Waziri wa ndani katika utawala wa zamani wa Mubarak, Habib al-Adly, na baadhi ya waliokuwa wakuu wa usalama waliokuwa wameshitakiwa kwa makosa sawa na Mubarak.

"Ni Historia pekee na mungu ndio anayepaswa kuitwa kutoa hukumu kwa mtu aliyeitumikia nchi hii kama Makamu wa Rais na kisha rais kwa miaka 30," alisema Jaji Mahmoud al-Rasheedi.

Katika kesi tofauti, Mahakama hiyo ilimuondolea makosa ya ufisadi Mubarak, watoto wake wawili wa kiume Alaa na Gamal, na mfanyabiashara tajiri nchini humo.

Aidha muda mfupi baada ya hukumu hiyo kutolewa wanaharakati waliandamana barabarani mjini Cairo lakini wakazuiwa na maafisa wa usalama kuingia katika uwanja wa Tahriri ambao ni ngome yalikoanza maandamano yaliodumu siku 18 na yaliomuondoa madarakani Hosni Mubarak.

Rais wa Zamani Hosni Mubarak
Rais wa Zamani Hosni MubarakPicha: AFP/Getty Images

Kulingana na ripoti za tovuti ya al-Masry al-Youm, polisi walitumia gesi ya kutoa machozi na kuwakamata baadhi ya waandamanaji. Utawala wa Misri uliuzunguka uwanja wa Tahrir ili kuzuwiya maandamano ya familia ya waathirika wa maandamano yaliopita na wanaharakati wanaotaka mageuzi.

Hata hivyo katika mji wa pwani wa Alexandria, polisi waliwatawanya waandamanaji wanaompinga Mubarak na kuwakamata wanne kwa makosa ya kuandaa mkutano wa hadhara bila ruhusa ya serikali.

Kundi la Udugu wa Kiislamu lasema uamuzi si wa mahakama si wa haki

Aidha kundi lililopigwa marufuku la Udugu wa Kiislamu limeuita uamuzi wa mahakama uliotolewa hapo jana Jumamosi kama hukumu ya kifo kwa raia wa Misri." Mahakama isingethubutu kutoa uamuzi kama huo, lakini imefanya hivyo kutokana na imani yake ya ulinzi inayopewa na utawala wa jeshi," lilisema kundi hilo lililo na itikadi kali, likiiangazia serikali ya rais Abdel-Fattah al-Sissi, mkuu wa zamani wa jeshi aliyeongoza kuondolewa kijeshi rais wa kundi hilo Mohammed Mursi mwaka uliopita.

Kwa upande wake Mmoja wa waandamanaji aliyekasirishwa na uamuzi wa mahakama amesema uamuzi huo si wa haki, na kwamba watu wa Misri hawastahili jambo kama hilo kutoka kwa mahakama hiyo baada ya kungoja uamuzi kwa muda mrefu.

Waandamanaji waliojawa na huzuni baada ya kusikia uamuzi wa kumfutia mashitaka Mubarak
Waandamanaji waliojawa na huzuni baada ya kusikia uamuzi wa kumfutia mashitaka MubarakPicha: picture-alliance/dpa/M. Kamal

Baada ya uamuzi huo baadhi ya wanaharakati wanasema huenda Mubarak akaachiwa hivi karibuni. Rais huyo wa zamani aliye na umri wa miaka 86 anatumikia kifungo cha miaka mitatu jela kwa makosa tofauti ya ufisadi.

Tangu kukamatwa kwake mapema mwaka wa 2011 Mubaraka amekaa muda wake mwingi katika hospitali ya kijeshi mjini Cairo kwasababu ya kudhoofika kwa hali yake ya afya. Aidha waliposikia uamuzi wa kuondolewa mashitaka kwa Mubarak, watoto wake wawili waliokuwa wako karibu naye waliamka wakambusu huku washitakiwa wengine wakikumbatiana.

Baadaye mamia ya wafuasi wake walikusanyika nje ya hospitali ya kijeshi Kusini mwa Cairo wakifurahia kufutiwa mashitaka kwa kiongozi wao. Akizungumza katika mahojiano ya chombo kimoja cha habari kilichotiifu kwa Hosni Mubarak, alisema kuwa alikuwa na uhakika wa kufutiwa mashitaka.

Hosni Mubarak
Hosni MubarakPicha: Reuters/A. Abdallah Dalsh

"Sikutoa maagizo ya kuuwawa kwa waandamanaji hata kidogo, nilingojea uamuzi huu kwa kumuamini mungu na kuamini kuwa sina hatia," alisema Mubarak alipokuwa anazungumza na kituo cha televisheni cha Sada al-Balad.

Mwaka wa 2011 Hosni Mubarak alihukumiwa kifungo cha maisha kwa kushindwa kuzuwiya mauaji ya waandamanaji na kuwa kiongozi wa kwanza wa Misri kufunguliwa mashitaka na kufungwa.

Aliyechukua nafasi yake Mohammed Mursi anayetokea chama kilichopigwa marufuku cha udugu wa Kiislamu naye amezuiwa akikabiiwa na mashitaka kadhaa ya uhalifu. Maelfu ya wafuasi wake wamekuwa wakiadamana mara kwa mara tangu alipoondolewa madarakani wakidai yeye ndio rais halali wa Misri aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia.

Mwandishi: Amina Abubakar/ dpa

Mhariri: Sekione Kitojo