Maandamano ya kupinga uchaguzi Msumbuji yageuka vurugu
25 Oktoba 2024Matangazo
Mamia ya wafuasi wa upinzani waliandamana, wakikataa kile walichokitaja kuwa kura iliyoporwa na tume ya uchaguzi "fisadi". Tume hiyo ilimtangaza mgombea wa Frelimo Daniel Chapo kushinda uchaguzi wa Oktoba 9 kwa asilimia 71 ya kura. Waandamanaji wamechoma moto matairi ya magari, kuziba njia mjini Maputo na kuharibu mabango ya uchaguzi ya Frelimo. Baadhi yao waliwarushia mawe polisi, ambao walirusha mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya, kwa mujibu wa ripota wa AFP. Kiongozi wa upinzani Venancio Mondlane aliyejitangaza kuwa mshindi amedai uchaguzi huo uligubikwa na udanganyifu na kuitisha maandamano.