Maaskofu waomba mwanga kuhusu kasoro za uchaguzi Kongo
4 Januari 2024Katika tangazo leo Alhamisi, makanisa hayo mawili pia yamemuomba mwendesha mashtaka mkuu wa korti ya katiba kufuatilia madai yote kuhusu visa vya kasoro hizo ili kufungua mashtaka dhidi ya wahusika na mapungufu hayo na visa vingine vya udanganyifu katika uchaguzi.
Tangazo hilo limejiri wiki moja baada ya tume yao ya pamoja ya uangalizi wa uchaguzi kutoa ripoti kuhusu uchaguzi uliofanyika hivi karibuni na ambao tume huru ya uchaguzi ilitoa matokeo Jumapili iliyopita. Makanisa hayo yanaomba kuundwe tume huru ya pamoja ili kutoa mwanga kwani ndio utakaorahisisha matokeo ya uchaguzi katika ngazi zote kukubaliwa.
Wagombea ambao hawakuridhishwa na matokeo walikuwa wamepewa muda wa siku mbili ili kuwasilisha mashauri yao mahakamani ila ni Théodore Ngoy ndiye mgombea pekee katika uchaguzi wa urais aliyewasilisha shauri lake mbele ya mahakama ya katiba. Kwa upande mwengine tume ya uchaguzi CENI imeamua kuahirisha kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa wabunge wa kitaifa ikieleza kwamba bado inaendelea kupokea na kujumuisha kura.