MABINGWA WA DUNIA BRAZIL WAKUMBANA JUMAPILI HII NA ARGENTINA KATIKA FINALI YA COPA AMERICA.KOMBE LA KLABU BINGWA BARANI AFRIKA-ENYIMBA INA MIADI NA BAKILI BULLETS YA MALAWI NA MAREKANI YACHANGIA KIKOSI CHA ASKARI 400 KWA OLIMPIK ATHENS.
22 Julai 2004MICHEZO WIKI HII:
Katika kinyan’ganyiro cha Kombe la klabu bingwa barani Afrika, Jumapili hii , mabingwa Enyimba wa Nigeria wanaikaribisha nyumbani Bakili Bullets ya Malawi.Enyimba ilipindukia matarajio ya mashabiki wake ilipotamba mbele ya Africa sports ya Ivory Coast kwa kuizaba mabao 3-0 mjini Abidjan, nyumbani mwao. Siku moja kabla ,Bakili Bullets ya malawi ilipatwa na msukosuko kwa kukomewa bao 1:0 nyumbani na Etoile du Sahel ya tunisia.Kwavile Etoile inatumainiwa kutamba nyumbani katika kundi A, klabu za Nigeria na tunisia zaweza kujikuta katika nafasi bora zikiwa zimechezwa duru 2 tu kati ya zote 6 za kinyan’ganyiro hiki.
Enyimba kutoka Aba,mji wa kusini-mashariki mwa Nigeria,ilianza kuja juu baada ya kubadili kocha ilipoachana na Milorad Urukalo na kumuajiri Felix Emordi.
Bullets,mfadhili wao ni mwendawazimu wa mpira rais wa zamani wa malawi-Bakili Muluzi nae ameapa kuifanya timu hii ya malawi kuwa mojawapo ya klabu kali kabisa barani Afrika.Lakini ikiwa Enyimba, itatia tena fora kama ilivyofanya mjini Abidjan ilipoitimba Africa Sports kwa mabao 3-0, risasi za Bakili Bullets zitakua za mpira tu hazina dhara.
Etoile du Sahel ya tunisia, baada ya kuibuka mabingwa wa Kombe la washindi na la shirikisho la CAF la Afrika mara 2 na mara moja Kombe la Suzper Cup la Afrika,wana uchu sasa wa kulitwaa Kombe hili la klabu-bingwa baada ya kuvunjwa moyo katika majaribio 6 yaliopita.Na katika uwanja wao wa olimpik ,Etoile ni vigumu kutiwa munda na ,kuangushwa mjini Sousse kandoni mwa bahari ya Mediterranian.
Esperence inaingia leo uwanjani na mahasimu wao ni wasenegali-Jean d’Arc.
Nani atakuwa kocha wa timu ya Taifa ya Ujerumani?:Taarifa za wiki hii mshambulizi wa zamani wa Ujerumani, Jürgen Klinsmann ndie atakaechukua usukani wa timu hiyo ya Taifa ulioachwa na Rudi Völler kufuatia kupigwa kumbo duru ya kwanza kwa Ujerumani katika Kombe lililopita la Ulaya nchini Ureno.
Klinsmann, ameripotiwa kusema,
"Nimefurahishwa kuona Shirikisho la dimba la Ujerumani limeridhia ombi langu la kujitolea kuisaidia timu ya taifa ya Ujerumani katika maandalio yake ya kombe lijalo la dunia 2006 nchini Ujerumani,"-alisema Klinsmann.
Mwenyekiti wa Shirikisho la dimba la Ujerumani Mayer-Vorfelder na makamo wake Werner Hackmann walikutana na Klinsmann juzi jumaane mjini New York-DFB ilisema.
Klinsmann alieichezea Bayern Munich, Stuttgart na Tottenham Hotspur ya uingereza, ana Leseni ya ukocha, lakini bila ya maarifa.Aklikuwa katika ile timu pamoja na Rudi Völler,ilitwaa Kombe la dunia 1990 mjini Roma,chini ya kocha Franz Beckenbauer.
COPA AMERICA:
Finali ya kombe la Amerika Kusini kesho itakua kati ya Brazil na jirani zake Argentina mjini Lima, Peru.Brazil ilitolewa jasho kabla kuitimua Uruguay kupitia changamoto ya mikwaju ya penalty. Uruguay ilitangulia kuufumania mlango wa Brazil kwa bao la kwanza la kichwa alilotia Marcelo Sosa mnamo dakika ya 22 ya mchezo.Adriano akasawazisha kwa Brazil dakika 2 baada ya kuanza kipindi cha mapumziko.Mwishoe, mikwaju ya penalty iliamua hatima ya timu hizo mbili.Brazil ilimtuliza shetani wake na kushinda mikwaju ya adhabu na kuitoa Uruguay kwa mabao 5-3.Brazil ilitia mabao yake yote 5 ya penalty.
Argentina maadui wa Brazil kesho, wanalitaka Kombe kwa kila hali mara hii ili kufuta dosari ya kupigwa kumbo duru ya kwanza ya kombe lililopita la dunia huko Korea na Japan baada ya kupigiwa upatu ingetawazwa mabingwa.
Kuingia finali ya kesho, Argentina iliitoa columbia kwa mabao 3:o kati ya wiki hii na ushindi huo dhidi ya mabingwa hao wa Amerika Kusini ulic hangia sana kuwarudishia heba yao ya miaka ya nyuma wakati wakicheza na Diego maradona.Mara ya mwisho kwa Argentina kutwa Kombe la Copa America ilikua 1993 na kesho wana miadi na mabingwa wa dunia-Brazil.Wanaamini kwamba, wataweza kuwika na kurejea na Kombe tena hadi Buenos Aires. Brazil itabisha.
Katika Kombe la dunia 1966 nchini Uingereza, mwanamxsumbiji Eusebio aliwika wakati mfalme Pele hakusikika.Chini ya Eusebio,Ureno iliipiga kumbo Brazil na mwishoe kuwasili nusu-finali ya Kombe lile la dunia.
Kati ya wiki hii Brazil ilimkumbuka mwanamsumbiji huyo ilipomtukuza kwa kuacha nyayo zake kandoni mwa chaki ya uwanja mashuhuri wa Maracana Stadium mjini Rio kama mastadi wengine wakubwa kabla yake kama mfalme Pele, wingi mashuhuri Garinca na Jaizinho.
Akiwa amezaliwa Msumbiji,koloni la zamani la Mreno,Eusdebio Ferreira da silva alikuwa stadi wa kwanza maarufu kutoka Afrika 1960.Mchezo wake wa kasi,jinsi ya kusarifu dim,ba na mikwaju yake mikali ilimfanya nyota yake kmunawiri wakati ile ya Pele ilififia katika Kombe la dunia,1966.
Eusebio aliibuka mtiaji magoli mengi kabisa katika Kombe hilo la dunia huko Uingereza-mabao 9.Eusebio aliibuka mtiaji mabao mengipia barani ulaya kwa klabu yake ya BENEFICA LISBON,1968 na 1973 .
KENYA wiki hii ilirejeshewa matumaini ya kuweza kurudi kucheza dimba la kimataifa mwezi ujao-alisema rais wa FIFA Sepp Blatter.Hii inafuatia mkutano wake Blatter na maafisa wa Kenya.FIFA ilisimamisha Kenya kucheza mashindano ya kimataifa mwezi uliopita kutokana na serikali ya Kenya kujiingioza ndani ya mambo ya chama cha mpira cha Kenya-kinyume na kanuni za FIFA.Kenya ilikosa kucheza mechi 3 za kanda ya Afrika kuania tiketi ya kuja Ujerumani kwa Kombe lijalo la dunia 2006.
TOUR DE FRANCE-mbio za baiskeli za Tour de France zinaingia katika hatua yake ya mwisho huku kila ishara ikibainisha kwamba, Lance Amstrong wa Marekani atatwaa mwishoe taji lake la sita la mbio hizi.Amstrong alikwishamkatisha tamaa hasimu yake mkubwa mjerumani Jan Ullrich alieangukia nafasi ya 4 kabla changamoto ya ljumamosi .Baada ya mbio hizi za baiskeli ijumaa kurejea bondeni ,ljumamopsi hii zinaingia katika hatua ya km 55 huko Basancoh ambako inatazamiwa kama ni duru ya heshima kwa Amstrong kabla kuvikwa taji lake la 6 la Tour de France.
MWISHOE MICHEZO YA OLIMPIK YA ATHENS:
Michezo ya olimpik ikikaribia kuanza rasmi hapo August 13,usalama unachangia sana maandalio ya michezo hii na ukila kitita kikubwa cha fedha za matayarisho.Ikiitikia ombi la Ugiriki,Marekani imejitolea kuchangia kikosi cha askari 400 kusaidia ulinzi katika michezo hii.Gharama jumla ya ulinzi imefikia dala bilioni 1.5.
Haikuamuliwa bado wapi kikosi hicho cha marekani kitawekwa kulinda usalama.Inafahamika kwamba Marekani inazungumza wakati huu na serikali ya Ugiriki kuhusu wapi kishike zamu.
Marekani ikiongoza katika kutoa madai kuwa vita dhidi ya ugaidi vienezwe hata katika michezo hii ya olimpik kufuatia hujuma ya Septemba 11, 2001,mjini washington na New York.