Macron afanya mazungumzo na Rais Xi Jinping mjini Paris
6 Mei 2024Macron alisalimiana na Xi katika kasri la Elysee, kabla ya kuanza mazungumzo yatakayogubikwa na vita vya Ukraine na mizozo ya kibiashara.
Duru ya kwanza ya mazungumzo itajumuisha pande tatu na kumshirikisha Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula Von der Leyen.
Macron amemweleza Xi kwamba ushirikiano na Beijing katika migogoro mikubwa ikiwemo Ukraine ni muhimu na kuhimiza kanuni sawa kwa wote katika uhusiano wa kibiashara baina ya China na Umoja wa Ulaya.
Rais Xi amesema mwanzoni mwa mazungumzo yake mjini Paris kwamba China inaichukulia Ulaya kama kipaumbele chake cha sera ya kigeni na kuutizama uhusiano kati ya pande hizo mbili kuwa wa kimkakati na endelevu.
Xi ameongeza kuwa China na Umoja wa Ulaya zinapaswa kuendelea kujitolea katika ushirikiano wa pande zote.