Macron akosa wingi wa kutosha bungeni
20 Juni 2022Ushindi mwembamba wa rais Emmanuel Macron na washirika wake ni matokeo yanayoonekana kuwa pigo kwa rais huyo aliyechaguliwa hivi karibuni kuongoza kwa awamu ya pili.
Ilitarajiwa kwamba muungano huo wa rais Emmanuel Macron wa Ensemble ungeibuka na idadi kubwa ya viti katika uchaguzi huo uliofanyika jana Jumapili, na kufuatiwa na muungano wa Nupes wa mrengo wa kushoto unaoongozwa na Jean-Luc Melenchon, hii ikiwa ni kulingana na utabiri wa awali.
Lakini hata hivyo, Macron na washirika wake wameanguka vibaya na kushindwa kujizolea wingi wa viti ili kuwa na uhakika wa kulidhibiti bunge. Hata mawaziri pamoja na wasaidizi wa karibu wamekiri hilo wakisema hawana namna nyingine zaidi ya kuwaendea walio nje ya muungano huo ili waweze kutawala taifa hilo.
Waziri wa fedha wa Ufaransa Bruno Le Maire ameyafananisha matokeo hayo na tetemeko la kidemokrasia na kusema watazungumza na upande unaounga mkono Ulaya kwa lengo la kujiimarisha zaidi kiutawala.
Mrengo wa kushoto wajiimarisha zaidi.
Muungano wa vyama vya mrengo wa kushoto wa Melenchon umeshuhudia ukijiimarisha mara tatu zaidi ikilinganishwa na uchaguzi wa bunge wa mwaka 2017, lakini hata hivyo wameshindwa kupata ushndi unaotakikana, ambao Melenchon pia aliutarajia.
Soma Zaidi: Chama cha Macron chashinda viti vingi bungeni
Iwapo itathibitishwa, bunge ambalo halijapata mshindi mwenye wingi wa kutosha wa viti litalazimika kuanzisha mchakato wa kisiasa ambao utahusisha pia mgawanyo wa mamkala miongoni mwa vyama vya siasa, hali ambayo haijashuhudiwa nchini Ufaransa katika miongo ya karibuni, ama kushuhudiwa mkwamo wa kisiasa na pengine raia wa taifa hilo watalazimika kurudi kwenye uchaguzi.
Kiongozi wa chama cha National Rally cha mrengo wa kulia Marine Le Pen alipozungumza na wafuasi wake kwenye mkutano wa hadhara jana Jumapili kufuatia matokeo hayo, amesema chama chake kimefanikiwa pakubwa kufanikisha lengo la kumfanya Macron kuwa rais wa wachache. Ikumbukwe kwamba Le Pen alikuwa mpinzani mkubwa wa Macron kwenye uchaguzi wa urais.
"Kumfanya Macron kuwa rais wa wachache ili kulilinda taifa letu dhidi ya utawala wa chama kimoja na rais aliyeshindwa kudhibiti mamlaka yake.", alisema Le Pen
Waziri mkuu wa Ufarasa Elisabeth Borne akizungumza kupitia televisheni amesema matokeo hayo yanaliweka mashakani taifa hilo na kuibua changamoto ambazo hawawezi kuzikabili, lakini akiapa kusaka ushirika haraka iwezekanavyo, kuanzia hii leo Jumatatu.
Muungano mpya wa mrengo wa vyama vya mkali wa kushoto, Soshalisti na Kijani unatarajiwa kuleta upinzani mkubwa ukiwa na kiasi viti 150 hadi 200 bungeni, huku National Rally kikitarajiwa kupata viti zaidi ya 80, kutoka vinane vya awali katika uchaguzi wa wabunge 577 wa bunge la Kitaifa nchini Ufaransa.
Macron, mwenye miaka 44 alichaguliwa kwa awamu ya pili katika uchaguzi wa mwezi Aprili lakini amerejea huku kukiwa na mpasuko mkubwa wa kitaifa kutokana na vyama vya mirengo ya kushoto na kulia kuzidi kupata umaarufu, na kwa maana hiyo kuweka kizingiti kikubwa katika juhudi zake za mageuzi zaidi kwenye taifa hilo la pili kiuchumi katika ukanda wa Euro.
Soma Zaidi:Macron ampiku Le Pen na kupata muhula wa pili
Mashirika: RTRE/AFPE