Madaktari 3 wakamatwa kwa mauaji ya daktari mwenzao DRC
8 Agosti 2019Matangazo
Mwendesha mashtaka wa makahama ya kijeshi nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesema madaktari watatu wamekamatwa na wanazuiliwa kwa tuhuma za mauaji ya daktari mmoja wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ambaye alikuwa ni miongoni mwa madaktari wanaopambana na mripuko wa homa ya Ebola.
Daktari huyo raia wa Cameroon, Richard Valery Mouzoko Kiboung, aliuawa kwa kupigwa risasi mnamo Aprili 19 kwenye shambulio katika hospitali moja katika mji wa Butembo mashariki mwa Kongo.
Mwendesha mashtaka wa kijeshi katika jimbo la Kivu Kaskazini, Luteni-Kanali Jean-Baptiste Kumbu Ngoma, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba madaktari waliokamatwa watashtakiwa kwa makosa ya ugaidi na jinai na kwamba bado kuna daktari mmoja ambaye bado anatafutwa.