1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiIndia

Madaktari nchini India wafanya mgomo wa kitaifa

17 Agosti 2024

Madaktari nchini India leo wameanza mgomo wa kitaifa na kuchochea maandamano zaidi baada ya ubakaji na mauaji ya kikatili ya mwenzao ambayo yamesababisha hasira iliyoangazia suala sugu la unyanyasaji dhidi ya wanawake.

https://p.dw.com/p/4jZwa
Wanafunzi wanaosemea udaktari nchini India wafanya mgomo Jumamosi 17,2024, kulalamika kuhusu mauaji ya mwenzao katika hospitali moja ya umma mjini Kolkata wiki iliyopita
Wanafunzi wanaosemea udaktari nchini India wafanya mgomo kulalamika kuhusu mauaji ya mwenzaoPicha: Ajit Solanki/AP Photo/picture alliance

Mjini Kolkata, maelfu ya watu walifanya mkesha wa kuwasha mishumaa hadi alfajiri ya leo Jumamosi. Bango moja lililobebwa na mwandamanaji lilikuwa na maandishi yaliosema ''mikono inayoponya haipaswi kuvuja damu.''

Daktari huyo aliyeuawa alipatikana katika ukumbi wa mafunzo wa hospitali hiyo, hali inayoashiria alikuwa ameenda kupumzika kabla ya kuendelea na kazi yake ambapo alikuwa zamu kwa masaa 36.

Uchunguzi wa maiti wathibitisha unyanyasaji wa kingono

Uchunguzi wa maiti ulithibitisha unyanyasaji wa kingono, na katika ombi kwa mahakama, wazazi wa mwathiriwa walisema walishuku binti yao alibakwa na genge la watu.

Mshukiwa mmoja wa mauaji akamatwa

Mwanamume mmoja, ambaye alifanya kazi ya kupanga watu kwenye foleni katika hospitali hiyo, amezuiliwa.

Hata hivyo, polisi mjini Kolkata wameshtumiwa na umma wenye hasira kwa kuendesha kesi hiyo vibaya na mahakama kuu ya mji huo ilihamisha uchunguzi wa kisa hicho kwa Ofisi Kuu ya Upelelezi ya India ili kudumisha imani ya umma.