Madaktari wa Nairobi waanza mgomo
21 Agosti 2020Mgomo wa madaktari hao ulioanza usiku wa manane huku maambukizi ya COVID 19 yakiongezeka, unayaweka maisha ya maelfu ya wagonjwa katika hatari baada ya mazungumzo kati ya chama chao na shirika la kutoa Huduma jijini Nairobi kusambaratika.
Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari na Wafamasia nchini Kenya tawi la Nairobi Daktari Maelo Deogratious anadai kuwa madaktari wanaohudumia wagonjwa wa COVID-19 hawana bima ya afya ilhali maisha yao yamo hatarini.
Fedha zilizotolewa na rais
Rais Kenyatta alitoa shilingi bilioni tatu kwa wizara ya afya, huku sehemu ya fedha hizo ikitakiwa kutolewa kwa bima ya madaktari. Madaktari hao wanadai kuwa hawajapokea fedha hizo.
Kwa mujibu wa chama cha Madaktari na Wafamasia jijini Nairobi hawajakuwa na bima ya afya tangu Julai mosi. Ripoti iliyotolewa na madaktari hao inasema kuwa baadhi yao walioambukizwa virusi vya corona walilazimika kugharamia matibabu yao walipokuwa wanaugua.
Aidha, wanadai kuwa hawajalipwa mishahara yao ya mwezi wa sita na saba. Maelo anasema kuwa jimbo la Nairobi halina eneo maalum la kuwatenga madaktari pamoja na wahudumu wengine wa afya ambao huambukizwa ugonjwa huo, wakiwahudumia wagonjwa, huku madaktari 15 wakiwa tayari wameuguwa virusi vya corona.
Mishahara yachelewa
Hata hivyo, Naibu Waziri wa Afya Mercy Mwangangi, anasema kuwa mishahara ya madaktari ilichelewa kwa sababu ya usimamizi mpya wa jiji.
Mazungumzo kati ya madaktari na serikali yamekuwa yakifanyika kwa kipindi cha miezi sita sasa na hayajafanikiwa. Madaktari watano wamepoteza maisha yao tangu janga la virusi vya corona lilipoingia nchini Kenya, huku idadi hiyo ikihofiwa kuongezeka.
Nusu ya idadi yote ya maambukizi ya virusi vya corona imeripotiwa katika jimbo la Nairobi. Kenya imerekodi zaidi ya visa 31,000 vya ugonjwa wa COVID-19, watu 17,800 wamepona huku idadi ya waliokufa ikizidi 500.