1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Madereva wa Safari Rally kuwalinda wanyamapori Kenya

9 Julai 2021

Serikali ya Kenya imewahimiza madereva wanaoshiriki mashindano ya kimataifa ya mbio za magari kushiriki juhudi za kulinda wanyama pori kwa minajili ya kuimarisha mazingira na utalii wa taifa hilo.

https://p.dw.com/p/3wI4v
Kenia | Kenya Wildlife Service
Picha: KWS

Wakati huo huo, wataalam wa kimazingira wanataka mikakati iwekwe kuhakikisha mashindano hayo ambayo yanatarajiwa kuendelea kwa miaka mingine tano, hayaondoi  mafanikio yaliyopatikana hatua katika kutunza mazingira.

Zoezi la kusafisha mazingira kwenye maeneo ambapo mashindano ya mbio za magari za safari rally yalifanyika hapa kaunti ya Nakuru limefikia kikomo, serikali ya Kenya ikisisitiza kwamba mashindano hayo hayakuathiri mazingira kwa njia yoyote. Serikali imetoa wito kwa madereva wanaoshiriki mashindano haya kushiriki jitihada za kuwalinda wanyama pori hasa wanaokabiliwa na tishio la kutoweka kutokana na uwindaji, uvamizi wa makaazi yao na mabadiliko ya tabia nchini. Patrick Omondi, Afisa msimamizi wa kitengo cha utafiti na mafunzo katika shirika la huduma kwa wanyama pori, KWS

Kenia | Kenya Wildlife Service
Patrick Omondi, Afisa mwandamizi wa shirika la KWSPicha: KWS

Kwenye zoezi la usafishaji lililoongozwa na maafisa wa shirika la huduma kwa wanyama pori, nyasi na miche elfu moja ya miti asili ilipandwa ili kupunguza athari ya kaboni inayotoka kwa magari, hii ikiwa sehemu ya miti milioni 19 inayopangiwa kupandwa. Jackson Kinyanjui, mtaalam wa mazingira kutoka shirika la Climate change Kenya ameelezea wasiwasi wa uchafuzi wa mazingira.

Rais Uhuru Kenyatta alitangaza kwamba Kenya itakuwa mwenyeji wa mashindano ya kimataifa ya mbio za magari kwa miaka mitano ijayo. Ingawa hili limepokelewa kwa hamu kubwa, swala la mazingira pia lafaa kupigwa darubini.

Mwanariadha mashuhuri kutoka Jamaica, Usain Bolt, alimuasili duma mwenye umri wa miezi mitatu alipozuru Kenya mwaka 2009. Bolt alilipa dola 13,700 ya kwanza, na malipo ya  kila mwaka ya USD 3000, yanayohitajika kumshughulikia mnyama huyo.

Wakio Mbogho, DW, Nakuru.