Maelfu waandamana Bangladesh kumtaka Waziri Mkuu kujiuzulu
28 Oktoba 2023Waandamanaji hao wanataka hatua hiyo ichukuliwe ili kuruhusu uchaguzi huru na wa haki chini ya serikali isiyoegemea upande wowote.
Maandamano hayo yanayotajwa kuwa ndiyo makubwa zaidi kwa mwaka huu yamevihusisha vyama vya Bangladesh Nationalist Party (BNP) na chama kikubwa cha Kiislamu cha Jamaat-e-Islami.
Takriban polisi 10,000 walisambazwa kuzuia ghasia kwenye maandamano hayo lakini wamepambana na mamia ya waandamanaji katika kitongoji cha Kakrail mbele ya kanisa kubwa la Kikatoliki, ambapo polisi wamelazimika kuwatawanya kwa mabomu ya machozi.
Waziri Mkuu Hasina, ambaye ni mtoto wa muasisi wa nchi hiyo, amekuwa madarakani kwa miaka 15. Licha ya ukuaji mzuri wa uchumi katika uongozi wake, mfumuko wa bei umeongezeka nchini humo. Serikali yake inatuhumiwa kwa rushwa na ukiukwaji wa haki za binadamu.