Maelfu wahofiwa kufa kwa kimbunga Mayotte
16 Desemba 2024Katika kisiwa hicho, idadi kubwa ya nyumba kwa maeneo tofauti zimeporokoka vibaya. Taswira kutoka Mayotte, zililionyesha matukio ya uharibifu wa kimbunga na marundo ya vifusi. Msemaji wa Idara ya ulinzi wa raia wa Ufaransa, Alexandre Jouassard amesema upepo mkali ulikuwa na nguvu za kipimo cha zaidi ya kph 200, umesababisha baadhi ya maeneo yashindwe kufikika.
Amesema kila dakika na saa inayoyoma ina umuhimu mkubwa katika juhudi za uokozi. Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron yupo katika mipango ya kufanya mkutano wa dharura wenye lango la kutafutia ufumbuzi mkasa huo. Shirila lenye wajibu wa masuala ya hali ya hewa la Ufaransa Meteo France limesema kimbunga hicho ni kikubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha zaidi ya miaka 90.
Athari inayoonekana katika viunga vya Mayotte baada ya kimbunga Chido
Mayotte ina wakazi wapatao 321,000 na inaundwa na visiwa viwili vikuu katika maeneo ya karibu ukiwa na ukubwa wa zaidi ya mara mbili ya Washington DC.
Kwa mujibu wa picha kutoka kwa vyombo vya habari vya ndani na Ufaransa, hali ilivyo kwa sasa ni kwamba mabaki ya mamia ya nyumba yanaonekana kutawanyika kando ya vilima, minazi mirefu imeanguka mapaa ya majengo, hospitali zilifurika maji.
Kiwango kamili cha majeruhi na uharibifu katika kisiwa hicho, ambacho kipo kati ya Madagascar na Msumbiji bado hakijafahamika. Ingawa inaelezwa inaweza ikawa mamia ya watu au pengine ikawa elfu kadhaa. Na kwamba pamoja na hayo kutakuwa na changamoto ya kupata takwimu halisi kwa kuwa baadhi ya familia zimekwisha fanya mazishi ya wapendwa wao.
Kitendawili cha idadi ya watu waliopoteza maisha
Mkuu wa kisiwa hicho anaelezea Francois Xavier Bieuville amenukuliwa akisema "Sitaweza kuhesabu idadi ya vifo, kwa sababu mila ya Waislamu ni kuzika watu ndani ya masaa 24, ambayo ni wazi mkuu wa Mayotte hatahoji. Na kwa hiyo, itakuwa vigumu sana kuwa na idadi ya mwisho. Lakini nadhani athari ni kubwa zaidi." Alisema ofisa huyo mwandamizi.
Soma zaidi:Kimbunga Chido chaipiga Msumbiji, kikitokea kisiwa cha Mayotte
Jean-Paul Bosland, ambae anaongoza shirikisho la kitaifa la wazima moto kwa Ufaransa amesema kwa Jumatatu hii uwanja wa ndege mkuu wa Mayotte, ulisalia kufungwa kwa raia kutofanya safari za ndege huku mashirika ya misaada ya kiutu yakiwa katika juhudi za kusaidia watu.
Chanzo: RTR