1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu wakimbia mapigano kati ya jeshi na M23

9 Desemba 2024

Mapigano yameendelea kuripotiwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kati ya jeshi la serikali na waasi wa M23, huku maelfu ya watu wakiyakimbia mapigano hayo yaliyokatiza safari za barabara ya Gomba-Butembo.

https://p.dw.com/p/4nuwN
DR Kongo Flüchtlinge aus Flüchtlingslager Kanyaruchikya
Picha: Benjamin Kassembe/DW

Vyanzo vya ndani vimeeleza kuwa mapigano hayo ya jana Jumapili yamezuka baada ya utulivu ulioonekana Jumamosi jioni katika vijiji vya Luofu, Miriki na Matembe ambako jeshi la Kongo lilishambuliwa kwa mizinga na waasi wa M23 wanaodaiwa kusaidiwa na jeshi la Rwanda.

Milio ya mabomu na silaha nzito yamesababisha hofu kubwa kwa wakaazi walioanza kuhangaika kwa wiki moja sasa.

Wakimbizi ni wengi na misaada hakuna

Baadhi wamekimbilia mji mdogo wa Kitsumbiro ulio umbali wa kilometa 20 kutoka eneo la vita wakibeba mizigo na mifugo yao, kama anavyoshuhudia hapa raia huyu.

Raia wakikimbia mapigano Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo
Raia wakikimbia mapigano Jamhuri ya Kidemokrasi ya KongoPicha: Benjamin Kassembe/DW

"Vita vinapamba moto kwenye mji mdogo wa Kaseghe. Jeshi linaendelea kukabiliana na waasi wa M23. Tatizo ni kwamba wakazi wanaokimbia kutoka Kaseghe na Miobwe wamekuwa wengi sana na hadi sasa hakuna msaada, hakuna dawa na hata maji safi. Imekuwa ni shida kubwa kabisa. Ni mambo magumu tunayoyapitia kwa sasa," alisema raia mmoja.

Hata hivyo, jeshi la Kongo, kupitia msemaji wake kwenye operesheni hizo, limedai kufanikiwa kuwazuia waasi wa M23 kusonga mbele kwenye vijiji vingine jirani na mji wa Kaseghe ambamo raia wote wamekimbia. Muhindo Simisi ni mbunge mchaguliwa wilayani Lubero anasema.

"Nchi ya Rwanda inaitesa Kongo sababu inalisaidia kundi la M23 na kulipa nguvu zaidi na hivi Rais Kagame anastahili kuchukuliwa mipango na kufikishwa mbele ya mahakama ya kimataifa, ICC. ili aulizwe kwa nini anaitesa Kongo. Anayefahamu magumu ya wanawake na watoto hata wazee afadhali awape uhuru Wakongo sababu ardhi hii ni yetu," alisema Muhindo Simisi.

Hadi Jumatatu, mji wa Kaseghe umekuwa chini ya udhibiti wa kundi la M23 huku jeshi la Kongo  likirudi nyuma takribani kilomita 10, vimeeleza vyanzo vya kiraia.

Pamoja na kukemea kutoshirikishwa kwao katika mazungumzo ya Angola, viongozi wa makabila mbalimbali mkoani Kivu Kaskazini wameleeza juu ya kile walichotaja kuwa njama ya kuivamia Kongo.

Tshisekedi na Kagame kukutana Angola

Mbele ya vyombo vya habari mwanzoni mwa juma lililopita, Joseph Nkinzo, afisa kutoka kundi linalowajumuisha viongozi hao wa makabila ameeleza hofu yake.

Rais wa DRC Felix Tshisekedi(kulia) akiwa na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame(kushoto)
Rais wa DRC Felix Tshisekedi(kulia) akiwa na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame(kushoto)Picha: Giscard Kusema

"Kumekuwa na mikataba mingi inayosainiwa kushoto na kuume na tumegundua kwamba inaweza kuliweka taifa la Kongo katika hatari kubwa sana. Ni lazima jambo hili lichukuliwe kwa umakini viongozi wa makabila yakishirikishwa," alisema Joseph Nkinzo.

Hali hii inajiri wakati ambapo Rais Felix Tshisekedi wa Kongo na Rais Paul Kagame wa Rwanda wanatarajiwa kukutana Desemba 15 nchini Angola kwa ajili ya mazungumzo yanayolenga kumaliza mzozo kati ya mataifa hayo mawili.

Mwandishi: Benjamin Kasembe