1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maafisa watano wa kukabiliana na ugaidi wauliwa Sudan

29 Septemba 2021

Idara ya ujasusi ya Sudan yasema maafisa wake wameendesha msako dhidi ya mtandao wa magaidi wanaofungamana na IS. Maafisa watano wa kupambana na ugaidi Sudan waliuwawa Jumanne wakati wa uvamizi uliofanyika Khartoum.

https://p.dw.com/p/411w8
Proteste Anti Islam Video Film Mohammed Karthum Sudan
Picha: Reuters

Idara ya ujasusi ya Sudan imetowa taarifa iliyogusia juu ya tukio hilo la jana Jumanne ikisema kwamba maafisa wa Ujasusi baada ya kupata taarifa kuhusu kuwepo kwa mtandao wa kigaidi unaofungamana na kundi la IS walianza kufuatilia kwa kufanya msako. Wakati wa operesheni hiyo ya msako maafisa wawili wa ujasusi  na wengine watatu wanaohusika na majukumu maalum waliuwawa wakati magaidi wanne raia wakigeni wakifanikiwa kukimbia. Kwa mujibu wa taarifa ya idara ya ujasusi ya Sudan magaidi 11 raia wa nchi mbali mbali walikamatwa kwenye msako.

Mwandishi habari wa shirika la AFP aliripoti kwamba jumba la ghorofa mbili iliyoko katika mji wa Jabra pembezoni mwa mji mkuu Khartoum ilizingirwa na kikosi cha walinda usalama walioutaka umati wa watu kuondoka kwasababu haikufahamika ikiwa magaidi hao waliacha mabomu kwenye jengo hilo.Majirani wa eneo hilo waliozungumza na shirika la habari la AFP walisema,walisikiamajibizano ya risasi na kushuhudia watu waliojeruhiwa wakisafirishwa kwa magari

Russland Dagestan Anti Terror Operation FSB Islamischer Staat
Picha: FSB/dpa/picture alliance

 Waziri mkuu Abdalla Hamdok ametuma salamu zake za rambi rambi kufuatia vifo vya maafisa hao watano wa ujasusi aliyowataja kuwa ni mashujaa waliouwawa wakipambana na kundi la watu wanaofungamanishwa na dola la kiislamu.Aidha waziri mkuu huyo pia amewatakia afwani ya haraka  wale waliojeruhiwa.

Mitandao ya propaganda ya kundi linalojiita dola la kiislamu haikutoa tamko lolote haraka linalotaja tukio hilo la Khartoum. Wakati kundi la IS halijawahi kusikika kuwa kitisho kikubwa nchini Sudan mnamo mwaka 2019 wizara ya mambo ya nje ya Marekani ilionya juu ya kitisho kinachosababishwa na makundi ya Jihadi nchini Sudan. 

Tahadhari hiyo ya Marekani iliweka wazi kwamba licha ya kutokuwepo kwa mashambulizi  ya kufanywa na makundi maarufu ya kigaidi,mitandao ya inayoratibu shughuli za IS inaonesha kuwepo ndani ya Sudan.Ripoti ya Marekani ya mwaka 2019 kuhusu ugaidi nchini Sudan ilibaini kwamba kundi mtandao huo wa IS iliitumia jina tafauti katika shughuli za kundi hilo.Aidha ripoti hiyo iliongeza kusema kwamba maafisa wa Sudan walikiri kwamba yapo makundi ya itikadi kali yanayohusishwa na IS katika nchi yao.

Sudan | nach Putschversuch | Premierminister Abdalla Hamdok
Picha: AFP/Getty Images

 Ikumbukwe kwamba upande wa Kaskazini mwa Sudan inapakana na Misri nchi ambayo kwa miaka inapambana na uasi kati rasi yake ya Sinai,uasi unaoongozwa hasa na tawi la IS nchini Misri. Juu ya hilo kundi jingine la wapiganaji wa itikadi kali linaendesha shughuli zake nchini Yemen ambayo ni kuvuka bahari ya Sham kutoka Sudan.

Pia kuelekea kaskazini na Magharibi IS linaendesha hujuma zake kwenye eneo pana ambalo halina uimamizi la mipaka ya maeneo ya jangwani ya nchi za Libya na Chad,likijumuisha wapiganaji kutoka kile kinachoitwa dola la kiislamu katika ukanda wa jangwa la Sahara-ISGS.

 

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW