Magazetini: Mtandao wa madanguro haramu Ujerumani wakamatwa
19 Aprili 2018Mhariri wa gazeti la Leipziger Volkszeitung anazungumzia kuhusu msako uliofanywa na polisi nchini Ujerumani dhidi ya makundi ya watu wanaofanya biashara ya kuwasafirisha watu kinyume na sheria na kuwatumia katika madanguro ya ukahaba nchini Ujerumani. Mhariri anaandika:
Katika msako mkubwa kabisa katika historia yake polisi ya Ujerumani ilikamata mtandao wa madanguro, ambayo yaliwaajiri watu waliobadilisha jinsia na kuwaingiza nchini Ujerumani kufanya kazi ya ukahaba kwa nia ya kujipatia fedha na kuwaingiza nchini humo kwa njia ya kuwapatia visa za kitalii kutoka Thailand. Nchi hii ya Thailand ambayo ni kivutio kikubwa cha utalii kwa watu wanaotaka kwenda katika mapumziko ya likizo, imejiweka katika taswira mbaya ya kuwa uwanja wa biashara ya haramu ya kimataifa ya kusafirisha binadamu.
Kuhusu mada hiyo hiyo mhariri wa gazeti la Neue Osnabrücker Zeitung, anaandika kwamba msako mkubwa umefanyika dhidi ya mtandao wa madanguro. Mhariri anaandika:
Biashara ya kusafirisha watu kwa njia haramu, ukahaba wa kulazimishwa, haya ni maneno mazito, ambayo yanajihusisha zaidi na picha zinazolingana na hali hiyo. Hii si mada ya kuipuuzia. Lakini pia ni lazima kutofautisha. Sio kila mwanamke, ambaye anapata fedha kwa kutumia mwili wake, analazimishwa. Kwa kuwa katika nchi hii kwa kiasi kikubwa ukahaba ni jambo linaloruhusiwa kisheria na kwa kuwekewa sheria maalum kuna uwazi katika shughuli hiyo. Ni muhimu basi kusisitiza kwa hiyo, kutojitumbukiza katika hatua ambazo si lazima kuzichukua. Hata hivyo kuchukua hatua dhidi ya biashara haramu ya kuwasafirisha watu kama ilivyo hivi sasa si hatua mbaya. Kwa sababu kuna upande uliojificha katika biashara hii ya ukahaba. Wanawake na wanaume wanalazimishwa kwa kutumia nguvu, kujiuza.
Jamii ya Kiyahudi ni sehemu ya jamii ya Wajerumani tangu enzi na enzi. Anaandika mhariri wa gazeti la General-Anzeiger la mjini Bonn, anapoandika maoni yake kuhusu mashambulizi dhidi ya Wayahudi nchini Ujerumani. Mhariri anaandika:
Tangu wakati huo jamii hii imekuwa mara kwa mara ikikabiliwa na chuki dhidi yake, madharau na kuwatoa thamani. Wanafunzi na waalimu wanapaswa kuwa na uwezo wa uvumilivu na maridhiano zaidi na kunapotokea hali ya kutokuwa na uvumilivu na maridhiano wachukue hatua kali. Mashirika ya Waislamu na misikiti yanapaswa kuwa na msimamo wa wazi. Sheria zinapaswa kutumiwa na kuzuwia kila aina ya chuki.
Mhariri wa gazeti la Stuttgarter Zeitung anaandika kwamba uwajibikaji wa kihistoria kuihusu Israel uko katika msingi wa taifa na watu wake. Mhariri anaadika hayo kuhusiana na mada ya maadhimisho ya miaka 70 tangu kuundwa kwa taifa la Israel. Mhariri anaadika:
Lakini hii haina maana kwamba kila njia ambayo serikali yoyote ya Israel inaamua kuchukua ni lazima kuiunga mkono. Hata hivyo Ujerumani pia ni lazima ichukue tahadhari kuhusiana na ongezeko la chuki dhidi ya Wayahudi na pia kutilia maanani ongezeko la siasa kali za mrengo wa kulia. Ubalozi wa Israel nchini Ujerumani ni muhimu hivi sasa kuliko wakati wowote ule.
Mwandishi: Sekione Kitojo / inlandspresse
Mhariri: Josephat Charo