Magufuli kuhitimisha kampeni za Dar es salaam
14 Oktoba 2020Mgombea urais wa CCM, Rais John Magufuli ambaye mwishoni mwa wiki alianza ngwe nyingine ya kampeni kwa kuyazungukia maeneo ya jiji la Dar es salaam, amesema serikali yake inakusudia kulisuka upya jiji la Dar es salaam iwapo atachaguliwa kukamilisha awamu yake ya pili ya uongozi.
Ametumia sehemu kubwa ya mikutano yake ya kampeni kutaja namna alivyofanikisha kukamilisha miradi ya ujenzi wa miundombinu kama vile barabara za kawaida na zile za mzunguko zinazojulikana kama flyover.
Jumatano akiwa katika Jimbo la Kawe jijini Dar es Salaam, ambalo mbunge wake ni kutoka chama cha upinzani Chadema, Rais Magufuli ametumia muda mwingi kuwanadi wagombea ubunge wa chama chake na kuwasihi wapiga kura kutomwangusha.
Mbali na hayo, Rais Magufuli amekumbusha misingi iliyowekwa na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, hasa ikiwa Tanzania inaadhimisha miaka 21 ya kifo chake.
Mgombea mwingine katika uchaguzi huu, Tundu Lissuwa chadema amesafiri hadi kisiwa cha Ukerewa kilicho katika ziwa Victoria mkoani Mwanza akilazimika kutumia usafiri wa mtumbwi kuvuka umbali wa kilometa 100 ziwani, baada ya kuelezwa kuwa boti inayotumiwa kuvusha abiria siku zote imeharibika.
Mwanasiasa huyo amekosoa kitendo hicho alichodai pengine kilikuwa na lengo la kukwamisha safari yake ya kwenda kuzungumza na wapiga kura kisiwani hapo.
Profesa Ibrahim Lipumba anayewania urais kupitia chama cha wananchi CUF, yuko katika kanda ya kati, mkoani Singida ambako aneendelea kukutana na wananchi akiwarai kumuunga mkono kwenye sanduku la kura hapo Oktoba 28.
Kwa hivi sasa wagombea wote wanaanza kupanga vyema mahesabu yao ya kampeni hasa wakati huu wanapoanza kuingia dakika za lalasalama katika uchaguzi wa mwaka huu. Ingawa tume ya taifa ya uchaguzi imeidhinisha jumla ya wagombea 15 wa urais hadi sasa ni wagombea watatu tu wanaondelea kusikika zaidi wakiyatawala majukwaa ya kampeni.