1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama Burundi yathibitisha hukumu kali kwa waandishi

Angela Mdungu
5 Juni 2020

Mahakama ya rufaa Burundi imeipitisha hukumu ya miaka miwili iliyotolewa kwa waandishi wanne wa habari amba walikuwa wamehukumiwa kwa makosa ya kuhatarisha usalama wa taifa.

https://p.dw.com/p/3dJfK
Burundi Bujumbura Pressekonferenz Journalisten
Picha: DW/J. Johannsen

Waandishi hao ni wafanyakazi wa shirika la habari la Iwacu ambalo ni moja kati ya mashirika machache binafsi katika taifa hilo la Afrika Mashariki.

Akizungumzia hukumu hiyo kupitia ukurasa wake wa Twitter kiongozi wa shirika la habari la Iwacu Antoine Kaburahe amesema "Tutaendelea kuitafuta haki hadi mahakama kuu. Tunawashukuru wote wanaotuunga mkono.”

Waandishi hao wanne waliohukumiwa, walikamatwa mnamo mwezi Oktoba mwaka uliopita katika eneo la Musigati wakati walipokuwa wakiripoti kuhusuhatma ya mapigano kati jeshi na kundi la waasi kutoka mkoa wa Kivu Kusini wa nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.  

Burundi Symbolbild Iwacu
Shirika la IWACU limesema litaendelea kutafuta haki kwa waandishi wake katika mahakama ya juu kabisaa.Picha: Getty Images/AFP/J. Huxta

Mwakilishi wa Kamati ya Kuwalinda Waandishi wa habari kusini mwa jangwa la Sahara, Muthoki Mumo amesema waandishi waliohukumiwa hawakupaswa kukamatwa kwa kufanya kazi yao na kwamba kesi hiyo haina kusudi jingine zaidi ya kulipa kisasi kwa waandishi wa habari.  

Burundi imekuwa na machafuko ya kisiasa tangu mwaka 2015, baada ya Rais Nkurunziza kutangaza kuwa atagombea muhula wa tatu wa urais. Alishinda uchaguzi wa marudio licha ya maandamano makubwa ambapo shirika la Umoja wa Mataifa linasema, zaidi ya watu 1,200 waliuawa.

Serikali ya Rais Pierre Nkurunziza ilivishughulikia vyombo vya habari kabla ya uchaguzi wa mwezi Mei ambapo mgombea wa chama tawala aliibuka mshindi. Vituo kadhaa vya redio na vyombo vingine vya habari vilifungwa na waandishi wengi wa habari waliikimbia nchi hiyo.

Rais huyo wa Burundi aliwashangaza wengi baada ya kutokugombea tena nafasi hiyo, lakini baadhi ya raia wa taifa hilo wana hofu kuwa anatumia mamlaka nyuma ya pazia akiwa kama "kiongozi wa juu wa chama tawala”

Chanzo: AFP