Mahakama ya kimataifa ICC yaanza uchunguzi dhidi ya mauaji ya Guinea
15 Oktoba 2009Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai, The Hague, imesema tayari imeanza uchunguzi wa awali dhidi ya mauaji hayo.
Uchunguzi huo wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai, unalenga katika kufafanua iwapo hujuma hizo zinaangukia katika mamlaka yake ya kisheria, pale ambapo vikosi vya walinzi wa rais, walipofyatua risasi kwa watu takriban 50,000 kwenye uwanja wa mpira wa miguu nchini humo mwezi uliopita.
Kikundi kimoja kinachojishughulisha na haki za binadamu nchini Guinea, kimesema katika tukio hilo watu 157 waliuawa, na wengine 1,200 kujeruhiwa vibaya, wakati serikali ya nchi hiyo inasema idadi ya watu waliouawa ni 57 tu.
Taarifa iliyotolewa leo na mwendesha mashtaka msaidizi wa mahakama imesema kuwa, wanawake walifanyiwa vitendo vya kikatili, na watu walionekana kuwa na mavazi ya kijeshi katika uwanja huo.
Mahakama hiyo imesema endapo itabaini kufanyika kwa hujuma hizo, basi itaanzisha uchunguzi rasmi, na wahusika watawajibika kwa mujibu wa sheria za kimatiafa.
Wakati Mahakama ya The Hague ikitangaza hatua yake hiyo, Kamishna wa Maendeleo wa Umoja wa Ulaya Karel de Gucht, ameyaita mauaji hayo, kuwa ni ukatili ambao haujawahi kushuhudiwa.
Karel de Gucht amesema hayo, mara tu baada ya kumaliza mkutano wake na maafisa wa Umoja wa Afrika, nchini Ethiopia.
Nayo Marekani imesema kuwa serikali ya kimapinduzi ya Guinea lazima iondoke madarakani, ili kupisha uchaguzi halali kufanyika, baada ya jeshi la nchi hiyo kuwaua maelfu ya waandamaji wa upinzani.
Msemaji wa Idara ya Nje nchini Marekani Phillip Crowley, amesema kuwa kwa mujibu wa majadiliano yaliyofanyika mjini Conakry na Washington, utawala wa kijeshi wa Kapteni Dadis Camara, lazima uondoke madarakani na kufungua milango kwa ajili uchaguzi huru, utakaoweka serikali halali itakayochaguliwa na watu wa Guinea.
Moussa Dadis Camara alitwaa madaraka mwezi Disemba mwaka jana, baada ya kifo cha rais wa wakati huo Lansana Conte, aliyeitawala nchi hiyo mzalishaji mkubwa wa madini ya asili ya aluminium, tangu mwaka 1984.
Waandamanaji hao walifyatuliwa risasi na wanajeshi wa nchi hiyo, baada ya hatua yao ya kupinga nia ya Kapteni Camara, ya kutangaza kugombea katika uchaguzi ambao utawala wake wa kijeshi umeupanga kufanyika mwezi Januari mwakani.
Navyo vyama vya kisiasa nchini humo, vimependekeza kuundwa kwa tume huru ya uchunguzi ya kimataifa, juu ya mauaji hayo.
Profesa Ansoumane Camara, wa Chuo Kikuu cha Conakry, na mchambuzi wa masuala ya siasa, akizungumzia juu ya pendekezo hilo la wapinzani, amesema:
"Itakuwa ngumu lakini huo ndio uwezekano wa pekee kwake na kwa watu wake.Moussa Didas Camara hatawali pekee yake bali anatawala pamoja askari wengi wenye usemi mkubwa. Sasa ameinama njia panda. Kwa hiyo Camara anapaswa kushauriana na askari wenzake juu ya mapendekezo yaliyotolewa na upande wa upinzani".
Mara kadhaa Camara amekaririwa akisema kuwa utawala huo wa kijeshi, upo madarakani kwa muda tu, ili kujaribu kupambana na rushwa pamoja na shughuli za usafirishaji wa madawa ya kulevya, kabla ya kuitishwa kwa uchaguzi wa kidemokrasia.
Mwandishi:Lazaro Matalange/AFP/APE
Mhariri:Abdul-Rahman.