Mahakama yamtia hatiani Trump kwa udanganyifu
27 Septemba 2023Chini ya Jaji Arthur Engoron, mahakama ya jiji la New York siku ya Jumanne (Septemba 26) ilisema imegunduwa kwamba Trump na kampuni yake walizidanganya benki, kampuni za bima na taasisi nyenginezo kwa kupandisha thamani kubwa zaidi mali zake kuliko ulivyo uhalisia na pia kutia chumvi juu ya utajiri wake kwenye nyaraka alizotumia kuingia mikataba ya kibiashara na kuchukulia mikopo.
Jaji Engoron aliamuru vibali vya baadhi ya biashara za Trump vifutwe kama ni adhabu kwake na bilionea huyo awekewe vikwazo ama kuzuiliwa kabisa kufanya biashara ndani ya jimbo la New York.
Soma zaidi: Je, Trump anataondolewa kuwania urais mnamo Januari 6?
Vile vile, jaji huyo aliamuru kuendelea kuwekwa kwa jopo maalum la kuchunguza kazi za kampuni ya Trump Organisation.
Trump: "Uamuzi yasiyo ya Kimarekani"
Mawakili wake walisema watakata rufaa dhidi ya uamuzi huo, ambao unamuondolea Trump uwezo wa kufanya maamuzi makubwa ya kimkakati na kifedha juu ya baadhi ya mali zake muhimu katika jimbo hilo.
Mwenyewe Trump alisema uamuzi huo wa mahakama unapingana na Umarekani na ni sehemu ya hujuma dhidi ya kampeni yake ya kurejea madarakani.
Soma zaidi: Harris: Trump hataachwa kuwajibishwa ghasia za Capitol Hill
Hadi sasa, rais huyo wa zamani wa Marekani mwenye umri wa miaka 77, anaongoza miongoni mwa wagombea wenzake wanaowania kuteuliwa na chama chake cha Republican kupigania urais katika uchaguzi wa mwaka 2024.
"Haki zangu za kiraia zimevunjwa, na mahakama ya rufaa, iwe ya shirikisho au ya jimbo, lazima iupitie uamuzi huu mbaya usio wa Kimarekani. Kampuni yangu imefanya kazi kubwa ya kusifika kwa jimbo la New York na imefanya biashara zake kikamilifu. Hakika hii ni siku ya huzuni sana kwa mfumo wa haki wa jimbo la New York." Aliandia bilionea huyo kupitia mtandao wake wa kijamii wa Truth Social.
Aendelea na kampeni
Kwa upande mwengine, Trump alikataa kushiriki kwenye mdahalo wa televisheni kati yake na wagombea wenzake wa urais kupitia Republican usiku wa Jumatano (Septemba 27), ambao aliuita ni onesho lisilo maana.
Hii ni mara ya pili kwa Trump kukataa kushiriki kwenye mdahalo, akiendelea kushikilia msimamo wake alioutowa mwezi Agosti, aliposema kwamba hana haja ya kupoteza wakati kwenye maonesho kama hayo wakati yeye ndiye anayeongoza kwenye kura za maoni.
Soma zaidi: Timu ya kampeni ya Trump yachangisha dola milioni 7.1 baada ya picha yake kusambazwa
Badala yake, siku ya Jumatano Trump alielekea Michigan kuzungumza na vyama vya wafanyakazi wa magari.
Jimbo hilo ni kiini cha sekta ya viwanda vya magari nchini Marekani na eneo ambalo lina ushindani mkali kati ya chama chake na cha Democrat cha hasimu wake, Rais Joe Biden.
Vyanzo: AFP, AP