Mahakama yamuidhinisha Nkurunziza Burundi
5 Mei 2015Mahakama hiyo imethibitisha uamuzi huo kupitia taarifa iliyotolewa Jumanne, huku maelfu ya waandamanaji wakimimika katika mitaa ya mji mkuu Bujumbura, kusema kamwe hawatokubaliana na uamuzi huo wanaoutaja kuwa kinyume na sheria.
Mwenyekiti wa chama tawala cha CNDD-FDD, Pascal Nyabenda, aliliambia shirika la habari la Uingereza Reuters kupitia ujumbe mfupi wa simu baada ya kuulizwa juu ya uamuzi wa mahakama, kuwa tayari mahakama hiyo imepitisha uamuzi wa kumuidhinisha rais Nkurunziza kugombea muhula wa tatu.
Uamuzi huo umekuja wakati makamu wa rais wa mahakama hiyo Jaji Sylvere Nimpagaritse, akiripotiwa kuikimbia nchi hapo jana, huku polisi nayo ikiwauwa waandamanaji watatu mjini Bujumbura, na kufanya idadi ya waliouawa katika muda wa wiki moja kufikia watu 13.
Gazeti la serikali ya Rwanda la New Times, liliripoti Jumanne kuwa makamu huyo wa rais wa mahakama ya katiba ya Burundi alikimbilia nchini Rwanda siku ya Jumatatu.
Jaji Nimpagaritse aliliambia shirika la habari la Ufaransa AFP, kuwa maoni ya wengi kati ya majaji saba wa mahakama hiyo waliamini itakuwa kinyume na katiba kwa Nkurunziza kusimama tena, lakini walikabiliwa na shinikizo kubwa na hata vitisho vya kuuawa kuwalaazimisha wabadili msimamo wao.
Marekani yaeleza wasiwasi
Nkurunziza, kiongozi wa zamani wa waasi kutoka kabila la walio wengi lam Wahutu, ambaye amakuwa madarakani tangu mwaka 2005, anakabiliwa na shinikizo kubwa kujitoa katika kinyanganyiro cha urais Juni 26. Katiba ya Burundi inasema mtu anaweza kuchaguliwa kuiongoza nchi hiyo kwa vipindi viwili tu vya miaka mitano
Waziri wa mambo ya Kigeni wa Marekani John Kerry alieleza wasiwasi kuhusiana na uamuzi wa Nkurunziza. "Tuna wasiwasi mkubwa kuhusu uamuzi wa rais Nkurunziza ambao unakwenda kinyume kabisaa na katiba ya nchi yake", alisema Kerry akiwa mjini Nairobi siku ya Jumanne, na kuongeza kuwa vurugu zinazoonyesha wasiwasi wa raia wake kuhusu chaguo hilo, zinapaswa kuzingatiwa na kuepushwa.
Baraza la Seneti la Burundi linalodhibitiwa na chama cha CNDD-FDD, liliiomba mahakama ya katiba kuamua juu ya suala hilo wiki iliyopita, lakini Nimpagariste alisema aliamua kutoweka sahihi yake kwenye uamuzi ambao hauna uhalali wowote wa kisheria na uliolaazimishwa kutoka nje, na hauna chochote halali juu yake.
Uamuzi huo uliyothibtishwa na taarifa ya mahakama, na kusainiwa na majaji sita, umesema hatua ya raia Nkurunziza ya kusimama kwa muhula wa tatu ambapo atachaguliwa na raia wote, haiendi kinyume na katiba ya Burundi. Kufuatia taarifa hiyo, waandamanaji kadhaa wameripuka mjini Bujumbura wakipiga za kelele na kusema kamwe hawatorushusu muhula wa tatu kwa raia huyo.
Rwanda yaionya Burundi
Nchi jirani ya Rwanda imeionya serikali ya Bunrundi na kuitaka iheshimu matakwa ya raia, ikieleza pia wasiwasi kuhusiana na ripoti kwamba waasi wa Kinyarwanda wanahusika katika vurugu hizo zinazopelekea maelfu ya wakimbizi kumiminika nchini Rwanda.
"Wakati tukiheshimu uhuru wa Burundi katika kushughulikia mambo yake ya ndani, Rwanda usalama wa raia wasio na hatia kama wajibu wa jumuiya ya kikanda na kimataifa," alisema waziri wa mambo ya kigeni Louise Mushikiwabo katika taarifa iliyotolewa siku ya Jumatatu.
"Rwanda inaitaka serikali ya Burundi kuchukuwa hatua zinazostahiki mara moja kuhakikisha inawalinda raia wake, kukomesha hali inayozidi kuwa mbaya ya kibinaadamu nam kurejesha amani," ilisema taarifa ya wizara ya mambo ya kigeni ya Rwanda.
Mushikiwabo alisema ana wasiwasi kuhusiana na ripoti kwamba vurugu nchini Burundi zinawahusisha waasi wa kabila la Wahutu walioko katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, maarufu kama Democratic Forces for the Liberation of Rwanda, FDLR.
Waasi hao wamekuwa wakiendesha shguli zao mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, katika mikoa inayopakana na Rwanda na Burundi -- tangu walipovuka mpaka kutoka Rwanda baada ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 ya watu hasa wa kabila la wachache la Watutsi.
Watu wasiopungua 24,000 wengi wao wakiwa wa kabila la Watusti wamekimbilia nchini Rwanda, wakihofia kuripuka kwa machafuko mengine ya kikabila, wamesema maafisa. Machafuko hayo yameitia wasiwasi hasa Rwanda, ambayo bado haijafuta kabisaa makovu ya mauaji ya mwaka 1994.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre,dpae,afpe.
Mhariri: Josephat Nyiro Charo