1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahamat rais mpya wa halmashauri kuu ya AU

Mohammed Abdulrahman30 Januari 2017

Umoja wa Afrika umepata rais mpya wa halmashauri kuu ya Umoja huo. Naye ni waziri wa mambo ya nchi za nje wa Chad, Moussa Faki Mahamat, aliyechaguliwa kwa  kura 39 kati ya 54 za nchi wanachama.

https://p.dw.com/p/2WfGd
Äthiopien Debatte der Präsidentschaftskandidaten der Kommission der Afrikanischen Union
Picha: DW/C. Wanjohi

Moussa Faki Mahamat, alizaliwa Juni 21 mwaka 1960 katika mji wa Biltime mashariki mwa Chad. Aliteuliwa kuwa Waziri mkuu Juni 2003 hadi Februari 2005, na ni mwanachama wa Chama cha Uokozi cha Kizalendo - Patriotic Salvation Movement. Kuazia 2007 hadi 2008 alikuwa rais wa Baraza la  Kiuchumi, Kijamii na  Kitamaduni, kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje mwezi Aprili 2008.

Bw Mahamat, alisoma sheria katika chuo kikuu cha Brazzaville katika Jamhuri ya Congo. Wakati Hissene Habre alipochukua madaraka Juni 1982, Mahamat alikimbilia uhamishoni na akajiunga na Baraza la Mapinduzi la Kidemokrasi lililoongozwa na Acheikh Ibn Oumar. Lakini hakurudi Chad wakati Acheikh alipojiunga na serikali ya Habre 1988. Ilikuwa ni baada ya Habre kupinduliwa na  Idriss Deby ndipo Mahamat aliporudi nyumbani Juni 1999.

Äthiopien Debatte der Präsidentschaftskandidaten der Kommission der Afrikanischen Union
Mkutano wa kilele wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika, EthiopiaPicha: DW/C. Wanjohi

Aliteuliwa Mkurugenzi mkuu wa  wizara mbili kabla ya  kuwa Mkurugenzi Mkuu wa  Shirika la Sukari la Taifa kati ya 1996 na 1999. Machi 1999 hadi Julai 2002 akateuliwa  kuwa Mkurugenzi wa Ofisi ya Rais Deby, na alikuwa mkurugenzi wa kampeni ya Deby wakati wa uchaguzi wa Rais Mei 2001

Mpinzani mkuu wa  Mahamat katika duru ya mwisho ya upigaji kura alikuwa  Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Kenya Bibi Amina Mohammed. Senegal pia ilikuwa na mgombea  mwana diplomasia wa siku nyingi, Abdoulaye Bathily, aliyetolewa katika duru ya awali. Wengine katika orodha ya wagombea watano walikuwa ni Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Botswana Pelonomi-Venson Moitoi na Agapito Mba Mokuy kutoka Guinea ya Ikweta. 

Nkosazana Dlamini-Zuma Amtseinführung Vorsitz Afrikanische Union
Aliyekuwa rais wa zamani wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika, Nkosazana Dlamini-ZumaPicha: picture-alliance/dpa/J. Prinsloo

Wote wawili walikataliwa na Viongozi Wakuu  wa Umoja wa Afrika, wakati wa mkutano wao wa kilele mjini Kigali – Rwanda Julai 2016, baada ya kushindwa kupata uungaji mkono wa theluthi mbili kura ya siri.

Rais mpya wa Halamshauri Kuu ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, anachukua nafasi ilioachwa na Bibi Nkosazana Dlamini-Zuma wa Afrika Kusini  aliyeshika wadhifa huo Julai 2012 akimpokea Jean Ping wa Gabon. Bibi Dhlamini-Zuma hakugombea tena .

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman

Mhariri: Yusuf Saumu