1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahasimu wa kisiasa watunisiana misuli uchaguzi mdogo Nakuru

4 Machi 2021

Chaguzi ndogo nchini Kenya zimeng’oa nanga siku ya Alhamisi, vurugu kati ya wanasiasa na maafisa wa polisi zikishudiwa katika eneo la London mjini Nakuru ambapo wanahabari wanne na mbunge walishambuliwa na kujeruhiwa.

https://p.dw.com/p/3qCCy
Wahl Nakuru Kenia
Picha: Wakio Mbogho/DW

Uchaguzi mdogo wa wadi ya London ulianza mwendo wa saa kumi na mbili asubuhi kama ulivyopangiwa, ila baada ya masaa machache purukushani iliibuka kati ya maajenti wa chama cha UDA ambao ni wafuasi wa naibu Rais Wiliam Ruto na maafisa wa usalama.

Maseneta Kipchumba Murkomen na Susan Kihika walisikika wakijibizana na naibu kamishna wa kaunti ya Nakuru Mofat Moseti, baada ya kuzuka purukushani.

Soma pia: Siasa za Kenya zachukua mkondo wa 2007

Purukushani hii iliibuka baada ya Mbunge wa Langata Nixon Korir kushambuliwa na watu kwa madai ya kutoa hongo kwa wapigaji kura zoezi lilipokuwa likiendelea. Wanasisa wenzake wamemtetea wakikana na kusema alikuwa msimamizi wa mawakala na alikuwa akifuatilia hali.

Wahl Nakuru Kenia
Wabunge na maseneta wakilumbana na askari polisi wakati wa uchaguzi wa wadi ya London, iliyoko Nakuru, Kenya, Machi 4,2021.Picha: Wakio Mbogho/DW

Mbio za farasi wawili

Maafisa wa polisi walifyatua mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya watu, hali ambayo ilisimamisha shughuli yote ya uchaguzi kila mmoja akikimbilia usalama wake. Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen amelaani matukio haya kama yanayoirejesha demokrasia ya Kenya nyuma.

"Hauwezi kuamini kwamba haya yanafanyika katika Kenya ya leo. Watu wengi wamejeruhiwa, yupo aliyepelekwa hospitalini. Wabunge wamejeruhiwa baada ya kushambuliwa na maafisa wa polisi pamoja na watu waliofandiliwa na baadhi ya wanasiasa.”

Soma pia:Uchaguzi wa mchujo Jubilee waahirishwa Nakuru

Wahl Nakuru Kenia
Polisi ikiwahoji raia wakati wa zoezi la kupiga kura katika uchaguzi mdogo wa wadi ya London, kaunti ya Nakuru, Machi 04, 2021.Picha: Wakio Mbogho/DW

Wanahabari wanne walishambuliwa na kujeruhiwa wakati wa fujo hizi. Mmoja alilengwa kwa jiwe, mwingine akatupiwa kitoa machozi mgongoni na wengine wakavamiwa na wafuasi wa wanasiasa waliowapiga na kuwapora. Ulinzi mkali wa polisi umeimarishwa kwenye maeneo ya kupigia kura mjini Nakuru.

Uchaguzi huu wa Nakuru umevutia zaidi ya wagombeaji 15 lakini kinyang'anyiro ni kati ya wagombea wa vyama vya UDA na Jubilee, mahasimu wa kisiasa kutoka chama tawala cha Kenya wanaoutumia uchaguzi huu kudhihirisha umaarufu wao.