Majimbo kadhaa ya Ujerumani kufunga shule zake
13 Machi 2020Hatua hizo zinachukuliwa katika kukabiliana na mripuko wa virusi vya corona nchini Ujerumani. Kituo cha televisheni cha n-tv nchini Ujerumani kimetangaza taarifa hiyo baada ya kumnukuu meya wa Berlin, Michael Mueller ambaye amesema shule zitakazoanza kufungwa Jumatatu ijayo ni zile za sekondari.
Wito umekuwa ukiongezeka nchini Ujerumani kuchukua hatua sawa na zile zilizochukuliwa na nchi jirani za Ulaya, kuzifunga shule ili kusaidia kupunguza kuenea kwa virusi vya corona, lakini kutokana na mfumo wa ugatuzi, ni serikali za majimbo pekee ndiyo zina mamlaka wa kutoa matamko kama hayo.
Shule kufungwa hadi Aprili
Aidha, majimbo ya Saarland na Bavaria yametangaza kuzifunga shule zote kuanzia Jumatatu ijayo. Jimbo la Bavaria limesema wanazifunga shule zote, chekechea na vituo vya kulea watoto hadi mwishoni mwa likizo ya sikukuu ya Pasaka, katikati ya mwezi Aprili kwa lengo la kukabiliana na janga la virusi vya corona.
Kwa upande wake jimbo la Saarland limesema litazifunga shule zote katika kukabiliana na kuenea kwa virusi hivyo vya COVID-19. Waziri Mkuu wa Saarland, Tobias Hans amesema kufungwa shule hizo ni hatua ya tahadhari kutokana na jimbo hilo kupakana na mkoa wa Grand Est ulioko kaskazini mashariki mwa Ufaransa.
Aidha, majimbo mengine matatu ya Ujerumani likiwemo la North Rhine Westphalia leo yanatarajia kuamua kuhusu kuzifunga shule zake. Hayo yanajiri wakati ambapo siku ya Ijumaa Ujerumani imetangaza kifo cha sita kutokana na virusi vya corona, huku watu 2,000 wakiwa wameambukizwa nchini humo.
Ufaransa nayo imesema itazifunga shule zote za msingi na sekondari pamoja na chekechea kuanzia Jumatatu ijayo. Ubelgiji na Ureno nazo zimetangaza kuzifunga shule zake, huku shule na vyuo vikuu nchini Italia zikiendelea kufungwa nchi nzima kutokana na taifa hilo kuathirika zaidi na virusi vya corona.
Nchi 15 Afrika zathibitisha visa vya virusi vya corona
Wakati huo huo, nchi za Kenya, Ghana na Gabon zimetangaza visa vya kwanza vya corona na hivyo kuifanya idadi jumla ya nchi zilizothibitisha kuhusu virusi hivyo barani Afrika kufikia 15.
Msemaji wa Shirika la Afya Duniani, WHO, Tarik Jasarevic amezitolea wito nchi zote duniani kushirikiana katika juhudi za kutafuta namna ya kupata suluhisho kuhusu virusi vya corona ambavyo vimetangazwa kuwa janga la kimataifa.
''Kwanza hatujui nini kitatokea katika siku zijazo, na kwa upande wetu hatupendi kutabiri kitakachotokea, lakini tunaangazia zaidi katika kupata suluhisho. Na tunaiambia kila nchi, tafadhali muendelee kuchukua hatua madhubuti na kutokata tamaa na nchi zinapaswa kujiambia kwamba: kwa hakika hatujui, kila mtu anaweza kupata virusi,'' alifafanua Jasarevic.
Ama kwa upande mwingine, Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau amejiwekea karantini ya wiki mbili, baada ya mkewe Sophie Gregoire Trudeau kuambukizwa virusi vya corona. Mwanadiplomasia wa Ufilipino anayefanya kazi katika kamati inayoshughulika na masuala ya kisheria kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York ameambukizwa COVID-19. Kisa cha mwanadiplomasia huyo kinakuwa cha kwanza kurekodiwa kwenye Umoja wa Mataifa.
(DPA, Reuters, DW https://bit.ly/3cVfbp2)