Makabila ya Darfur huenda yakavibadili vita Sudan
6 Julai 2023Tangazo la viongozi wa makabila saba ya kiarabu katika jimbo la Darfur lililotolewa katika video iliyochapishwa Jumatatu wiki hii limeibua hisia mseto huku wachambuzi wakitahadharisha juu ya kutanuka kwa mpasuko wa kikabila ambao yumkini ukasababisha machafuko zaidi. Viongozi waliwahimiza watu wao waasi na kuachana na jeshi na badala yake wajiunge na kikosi cha RSF kupambana na jeshi la Sudan.
Mchambuzi na mwandishi habari mkongwe wa Darfur, Abdelmoneim Madibo amesema tangazo hilo litakuwa na athari kubwa katika vita vya Sudan ambavyo vimesababisha vifo vya watu karibu 3,000. Akizungumza na shirika la habari la Ufaransa AFP Madibo amesema huko El Geneina kwa mfano, wito huo utaligawa eneo la Darfur Kusini kati ya jamii za waarabu na zisizo wa waarabu.
Soma zaidi: Makabiliano yapamba moto Sudan bila kuwepo dalili za maridhiano
Pande mbili zinazohasimiana katika vita vya Sudan kwa muda sasa zimekuwa zikiwashawishi vijana wa Darfur wajiunge na upande wao, eneo ambako asilimia 25 ya idadi jumla ya wakazi wa Sudan wanaishi. Hata hivyo wataalamu wanasema ingawa vita vya Sudan vimeshachukua muelekeo wa kikabila katika eneo la Darfur, bado athari zake hazijajitokeza kwa upande wa muundo wa vikosi vinavyopigana sasa mbavyo vinawajumuisha wapiganaji wa makabila ya kiarabu na wasio waarabu.
Hali ya kibinadamu yazorota Sudan
Wakati hayo yakiarifiwa hali ya kibinadamu inaelezwa kuzorota Sudan huku mzozo wa vita ukiendelea. Tangu mwanzo wa mwezi huu wa Julai, mapigano yamechacha huku pande zote zikifanya mashambulizi mengi ya kukabiliana katika mji mkuu Khartoumna viunga vyake. Watu 20 waliuliwa na wengine 20 wakajeruhiwa Jumanne wiki hii katika mashambulizi ya makombora. Mapigano makali pia yamewalazimu watu wengi kuyakimbia makazi yao.
Zeinab Mirghani ni mkazi wa Omdurman. "Watu wote wa familia yangu wameikimbia Sudan. Dada zangu na kaka zangu wote wameondoka. Nilipoteza makazi yangu mjini Khartoum. Yaliharibiwa katika vita."
Soma zaidi: Mapigano yaendelea nchini Sudan licha ya matumaini ya utulivu
Kwa mujibu wa taarifa ya shirika la uratibu wa misaada la Umoja wa Mataifa OCHA iliyotolewa Jumatano wiki hii mzozo wa Sudan ulikuwa umesababisha vifo 1,133 na majeruhi 11,796 kote nchini. Takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya uhamiaji IOM zinaonyesha watu wapatao milioni 2.23 wameyakimbia makazi yao nchini Sudan na watu 697,000 wamekimbilia nchi jirani kutafuta hifadhi.
Kando na hayo naibu mkurugenzi wa shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto UNICEF, Omar Abdi, ameliambia baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kwamba watoto zaidi ya milioni moja wamelazimishwa kuyahama makazi yao Sudan kutokana na vita na umoja huo umepokea ripoti kwamba mamia ya wengine wameuliwa na kujeruhiwa katika mgogoro unaoendelea.
(afp,ap)