1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Makabiliano yaongezeka mpakani mwa Israel-Lebanon

17 Oktoba 2023

Mvutano katika mpaka unaozozaniwa wa Israel na Lebanon unazidi kuongezeka na kuzusha wasiwasi wa kutokea mzozo mpana wa kikanda.

https://p.dw.com/p/4XcgO
Usalama mpakani mwa Israel na Lebanon
Wanajeshi wa Israel wakishika doria kando ya barabara karibu na mpaka kati ya Israel na LebanonPicha: Francisco Seco/AP/picture alliance

Kumekuwa na majibizano ya ufyatulianaji risasi baina ya Israel na wanamgambo wa kundi la Hezbollah nchini Lebanon katika siku za hivi karibuni. Makabiliano hayo yalianza muda mfupi baada ya kundi la wanamgambo la Hamas ambalo Marekani na Umoja wa Ulaya limeliorodhesha kuwa shirika la kigaidi, kufanya shambulio kubwa dhidi ya Isreal mnamo Oktoba 7. Siku iliyofuatia vyanzo nchini Lebanon viliripoti mashambulizi ya Isreal yaliyoelekezwa kusini mwa nchi hiyo huku maganda ya risasi yakianguka kwenye kijiji cha Khiam.

Soma pia: Israel yaharibu roketi iliyorushwa kutoka Lebanon

Kundi la Hezbollah la nchini Lebanon ambalo linaungwa mkono na Iran tangu wakati huo limedai kuhusika na mashambulizi kadhaa ya maroketi kaskazini mwa Isreal, huku jeshi la Isreal IDF nalo, likijibu mapigo kwa kuyalenga maeneo zaidi upande wa kusini wa Lebanon na kuwaua wanamgambo kadhaa wa Hezbollah.

Wapiganaji wa Hezbollah
Mpiganaji wa Hezbollah akiwa ameshikilia kombora la kutungua ndege kusini mwa Lebanon.Picha: Hussein Malla/AP/picture alliance

Makabiliano hayo ya hivi karibuni ndio makubwa tangu vita vya Lebanon vya mwaka 2006 ambavyo vilisababisha wanamgambo 250 wa Hezbollah na Walebanon zaidi ya 1,000 kuuawa sambamba na askari 160 wa Isreal. Kundi la Hezbollah ambalo linajiendesha kama chama cha kisiasa likiwa na viti zaidi ya 60 katika bunge la Lebanon, pia limekuwa na tawi la wapiganaji ambalo linamiliki idadi  kubwa ya maroketi pamoja na maelfu ya wapiganaji walio na uzoefu. Nchi kadhaa zikiwemo Marekani na Ujerumani linalitambua kundi hilo kuwa la kigaidi.

Makubaliano ya mipaka: Israel na Lebanon zakubaliana mipaka ya baharini

Kikosi cha muda cha Umoja wa Mataifa nchini Lebanon UNIFIL kilisema katika taarifa yake mnamo Oktoba 15 kwamba wameshuhudia "majibizano makali ya risasi baina ya Lebanon na Isreal" haswa baada ya makao yake makuu kwenye mji wa Naquora kushambuliwa vikali.

Mapema siku hiyo hiyo, kundi la Hezbollah lilidai kuhusika na shambulio la kombora dhidi ya Isreal na kumuua mwanaume mmoja katika mji wa mpakani wa Shtula. Kundi hilo lilisema kwamba shambulio hilo lilikuwa ni ulipaji kisasi wa shambulizi la Israel ambalo lilipiga kundi la waandishi wa habari karibu na kijiji cha Alma-al-Shaab. Mwandishi wa shirika la habari la Reuters aliuawa kwenye shambulio hilo na kuchochea shirika hilo lenye makao yake makuu jijini London kuanzisha uchunguzi. Waandishi wengine watano walijeruhiwa.

Mvutano wa Lebanon-Isreal
Gari la mwandishi wa habari likiungua katika shambulizi la makombora yaliyorushwa kutoka upande wa Israel kusini mwa Lebanon.Picha: Thaier Al-Sudani/REUTERS

Siku ya Jumatatu, jeshi la Isreal lilitangaza kwamba takribani jamii 30 zilizoko ndani ya kilometa 2 kwenye mpaka wake wa kaskazini na Lebanon zitahamishwa na kulitaja kuwa eneo la kijeshi.

Eneo la mpaka baina ya Lebanon na Israel bado limesalia kuwa tete na lenye kuzozaniwa huku makabiliano ya mara kwa mara yakizuka. Hata hivyo, hakuna mpaka rasmi baina ya nchi hizo mbili na badala yake kumekuwepo na mstari unaotambua mipaka unaoitwa mstari wa buluu, ambao una alama ya mapipa ya samawati.

Mpaka huo ulianzishwa na Umoja wa Mataifa katika miaka ya 2000 ili kuthibitisha kuondoka kwa vikosi vya Isreal katika maeneo yanayokaliwa kusini mwa Lebanon.