1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makosa ya upimaji wa corona yaigharimu Pakistan

17 Machi 2020

Pakistan imesema imethibitisha visa 19 vipya vya COVID-19 idadi iliyoongezeka mara mbili kwa siku mbili mfululizo na hasa kutokana na makosa yaliyofanyika wakati wa upimaji katika karantini ya wasafiri.

https://p.dw.com/p/3ZaEH
Deutschland Coronavirus
Picha: Getty Images/S. Gallup

Aidha Iran imewaachia huru kwa muda takriban wafungwa 85,000 ikiwa ni pamoja na wafungwa wa kisiasa kufuatia janga hilo. 

Visa hivi vya karibuni kabisa vinafanya idadi kufikia wagonjwa 195 nchini Pakistan na kuibua wasiwasi kuhusiana na makosa hayo ya kiupimaji ambayo sasa yanaligharimu pakubwa taifa hilo na sasa likijaribu kudhibiti kasi ya kusambaa.

Maelfu ya wapakistan, wengi miongoni mwao mahujaji, waliwekwa karantini katika wiki za karibuni katika mpaka wa Taftan unaopita mkoa wa Balochistan, kaskazini mwa nchi hiyo baada ya kurejea kutoka Iran, moja ya taifa lililoathirika pakubwa na virusi vya corona, ulimwenguni.

Hata hivyo, takriban watu 119 miongoni mwao wamekutwa wameambukizwa virusi hivyo wakati walipoingia kwenye maeneo mengine ya nchi hiyo, hii ikiwa ni kulingana na maafisa wa maeneo hayo. Msemaji wa mkoa wa Sindh Murtaza Wahaba amelaumu mazingira ya karantini waliyowekwa raia hao, akisema haikuwa karantini bali ulikuwa ni mzaha mtupu. Na sasa wanasambaza virusi kwenye mikoa ya Sindh na Khyber Pakhtunkhwa.

Pakistan Coronavirus Covid
Picha: Reuters/F. Aziz

Bado kuna watu zaidi ya 500 wanatakiwa kusafirishwa kupelekwa Sindh, hali inayoibua kitisho cha kusambaa zaidi kwa maambukizi. Jana jioni waziri mkuu Imran Khan alielezea wasiwasi wake kuhusu virusi hivyo vitakavyodhoofisha zaidi uchumi wa mataifa ya ulimwengu wa tatu na kuathiri sekta ya afya, huku akiyarai mataifa tajiri kufikia kuwapunguzia mzigo wa madeni.

"Kutokana na athari za kuzorota kwa uchumi, hofu yangu ni umasikini na njaa. Hayo yananitia wasiwasi mkubwa kwa sasa, na kutokana na hilo nadhani, jumuiya ya kimataifa inapaswa kufikiria aina fulani ya kuwafutia madeni mataifa kama yetu, yaliyoko hatarini zaidi, angalau hilo litatusaidia kupambana na corona."   

Nchini Iran wafungwa takriban 85,000 ikiwa ni pamoja na wafungwa wa kisiasa wameachiwa katika harakati za taifa hilo kukabiliana na kusambaa virusi hivyo. Msemaji wa mahakama Gholamhossein Esmaili amesema hii leo kwamba hadi sasa tayari wafungwa hao wameachiwa, lakini pia wamechukua hatua kadha wa kadha za tahadhari magerezani kote nchini humo. ambako tayari idadi ya vifo imefikia 988.

Soma Zaidi: WHO: Dunia imeingia hali ya mashaka kufuatia virusi vya Corona

Iran ilitangaza kuwaachia wafungwa 70,000 mwezi Machi. Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya haki za binadamu nchini humo Javaid Rehman amesema ameiomba Tehran kuwaachia kwa muda wafungwa wote wa kisiasa kutoka kwenye magereza yake yaliyofurika na yanayokabiliwa na maradhi ili kusaidia kuzuia kusambaa zaidi kwa virusi vya corona.

Na huko Tokyo naibu mkuu wa kamati ya Olimpiki nchini Japan, Kozo Tashima hii leo amebainika kuambukizwa  virusi vya corona, katika wakati ambapo maafisa wa serikali wakisisitiza kwamba michezo hiyo itaendelea kama ilivyopangwa na kuruhusu mashabiki, huku kukiwa na ongezeko la wasiwasi kuhusu iwapo michezo hiyo itafanyika kama ilivyopangwa kufuatia kusambaa kwa virusi vya corona duniani.

Mashirika: RTRE