1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano kudhibiti gesi zenye kuchafuwa sana mazingira

15 Oktoba 2016

Takriban mataifa 200 yafikia makubaliano Jumamosi (15.10.2016) kudhibiti matumizi ya gesi zenye kuathiri mazingira ambazo zina nguvu kubwa kuliko hata hewa ukaa ikiwa ni hatua kubwa kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.

https://p.dw.com/p/2RGmA
Ruanda Kigali internationales Treffen zum Klimawandel
Picha: picture-alliance/AP Photo

."Ni hatua kubwa sana mbele " amesema hayo waziri wa mambo ya nje wa Marekani ambaye ameshiriki mazungumzo hayo yaliofanyika katika mji mkuu wa Kigali nchini Rwanda  " Jambo hili litatuwezesha kupunguza kiwango cha ujoto duniani kwa nyuzi joto nusu."

Mazungumzo kuhusu gesi mchanganyiko ya hewa ukaa, naitrogini na haidrogini au UFC unahesabiwa kama mtihani wa kwanza duniani tokea kufikiwa kwa makubaliano ya kihistoria huko Paris kupunguza utowaji wa gesi ya hewa ukaa hapo mwaka jana.Gesi hizo zinatajwa kuwa ni vichafuzi vya mazingira zinazoongezeka kwa haraka kabisa duniani na hutumika katika majokofu na viyoyozi.Wataalamu wanasema kuzipunguza gesi hizo ni njia ya haraka kabisa ya kupunguza kiwango cha ujoto duniani.

Ufumbuzi mkubwa

Ruanda Kigali internationales Treffen zum Klimawandel John Kerry
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani akizungumza Kigali.Picha: picture-alliance/abaca

Rais Barack Obama wa Marekani katika taarifa aliyoitowa Jumamosi ameyaita makubaliano hayo mapya kuwa "ufumbuzi mkubwa unaokwenda mbali sana katika kukabiliana na tatizo hilo la mabadiliko ya tabia nchi." Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameyaita makubaliano hayo kuwa "muhimu sana".Makubaliano hayo ambayo tafauti na makubaliano makubwa yaliofikiwa Paris utekelezaji wake ni wa kisheria.

Yanadhibiti na kupunguza matumizi ya gesi hizo katika mchakato wa hatua kwa hatua kuanzia mwaka 2019 kutakakofanywa na nchi zilizoendelea ikiwemo Marekani nchi inayoshika nafasi ya pili duniani kwa kuchafuwa mazingira.Zaidi ya nchi 100 zinazoendelea ikiwemo China mtowaji mkuu wa hewa ukaa duniani zitaanza kuchukuwa hatua ya kupunguza gesi hizo hapo mwaka 2024 wakati matumizi ya gesi hizo yatakapokuwa yamefikia kilele.

Kundi dogo la nchi zikiwemo India, Pakistan na baadhi ya mataifa ya Ghuba wameshinikiza kuanza kuchukuwa hatua mwaka 2028 kwa hoja kwamba uchumi wa nchi zao unahitaji muda zaidi kuendelea kukua.Mjumbe mkuu wa India taifa linaloshika nafasi ya tatu kwa kuchafuwa mazingira duniani Ajay Narayan Jha amesema "ni wakati wa kihistoria na wote wana furaha kwamba wamefikia nukta hiyo ambapo wameweza kufikia muafaka na kukubaliana takriban na masuala yote yaliowasilishwa mezani." 

Kupunguza kwa nyuzi joto nusu

Ruanda Kigali internationales Treffen zum Klimawandel John Kerry
Wajumbe wakimsikiliza waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry mjini Kigali.Picha: picture-alliance/abaca

Makundi ya kutetea mazingira yalitaraji makubaliano hayo yangeliweza kupunguza kiwango cha ujoto duniani kwa nyuzi joto nusu kufikia mwishoni mwa karne hii.

Rais wa taasisi ya masuala ya Utawala na Maendeleo Endelevu Durwood Zaelke amesema makubaliano hayo yamepiga hatua kama asilimia tisini kufikia lengo hilo.Taasisi hiyo ya Zaelke imesema upunguzaji huyo wa ujoto ni mkubwa kabisa kufikiwa katika makubaliano ya mara moja.

Inakadiriwa kwamba makubaliano hayo yatapunguza viwango vya dunia vya gesi hizo za HFC kwa asilimia 80 hadi 85 ifikapo mwaka 2047. Wataalamu wanataraji nguvu za masoko zitasaidia kuharakisha vikomo vilivyokubaliwa katika makubaliano hayo.

Mwandishi : Mohamed Dahman/dpa/AP 

Hariri : Sylvia Mwehozi