Makubaliano mapya ya kusitisha mapigano Ukraine yafikiwa
19 Februari 2017Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema hatua ya usitishaji mapigano kati ya waasi wanaoungwa mkono na Urusi na Jeshi la Ukraine itaanza hapo kesho Jumatatu. Kauli ya Lavrov inafuatia makubaliano yaliyofikiwa Jumamosi kati ya Ukraine, Urusi, Ujerumani na Ufaransa katika mkutano wa kimataifa wa usalama mjini Munich.
Akizungumza na waandishi wa habari pembezoni mwa mkutano huo, waziri huyo wa mambo ya nchi za nje wa Urusi amesema hiyo ni hatua nzuri kufuatia mawaziri wa mambo ya nje wa nchi nne kufikia makubaliano kwa mara nyingine kwa ajili ya kuanza hatua hiyo ya usitishaji mapigano Februri 20.
Makubaliano mapya yatafanikiwa?
Amesema makubaliano hayo pia yanahusisha kuanza kundolewa silaha nzito za kivita mashariki mwa Ukraine. Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel amesema mikutano mingine imepangwa kufanyika katika wiki zijazo ili kuhakikisha hatua hiyo ya usitishaji mapigano inatekelezwa.
Hata hivyo licha ya Lavrov kueleza kuwa mazungumzo hayo yamekuwa na tija, waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Pavlo Klimkin amesema hajafurahishwa na yaliyofikiwa katika mazungumzo ya Jumamosi na ameonya kuwa sharti yawe zaidi ya maneno matupu ya kisiasa akiongeza lazima ukweli halisi uliopo mashariki mwa nchi yake uzingatiwe la sivyo kutakuwa na duru nyingine ya mazungumzo.
Makubaliano mapya ya kusitisha vita yanakuja baada ya kiasi cha watu 30 kuuawa katika mapigano yaliyozuka upya mapema mwezi huu katika mzozo huo wa mashariki mwa Ukraine ambao umesababisha vifo vya zaidi ya watu 10,000 tangu ulipoanza mwezi Aprili mwaka 2014.
Waasi wanaotaka kujitenga wa kwa eneo hilo la mashariki mwa Ukraine wanaoungwa mkono na Urusi wamekataa kuthibitisha iwapo wanapanga kuyaheshimu makubaliano hayo mapya ya kusitisha mapigano huku baadhi yao wakisema wana mashaka iwapo inawezekana kuyatekeleza makubaliano hayo kuanzia Jumatatu
Kiongozi wa waasi wa jimbo la Donetsk Eduard Basurin amesema kumekuwa na mapigano makali siku nzima Jumamosi na haoni haja ya kutangaza usitishaji mapigano kutokana na hali ilivyo sasa akiongeza kwa upande wa wanajeshi wa serikali, hawaonekani kuondoka kutoka eneo la mapambano wala kuondoa silaha nzito kama ilivyokubaliwa katika makubaliano hayo.
Makubaliano yamekuwa yakikiukwa
Makubaliano kadhaa yaliyofikiwa katika kipindi cha nyuma ili kusitisha mapigano na kutafuta amani Ukraine yamekiukwa.
Mnamo mwezi Februari mwaka 2015, Ujerumani, Ufaransa, Urusi na Ukraine zilifikia makubaliano ya amani ya Minsk ambayo yalinuia kusitisha mapigano, kuondolewa kwa silaha nzito kutoka eneo la mapambano na marekebisho ya katiba yakaipa eneo la mashariki mwa Ukraine mamlaka zaidi ya kujitawala.
Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean Marc Ayrault amesema saa nyingine inabidi wakiri kuwa hakuna nia njema ya kuumaliaza mzozo huo kutoka kwa pande zinazozana Ukraine.
Huku hayo yakijiri, Rais wa Urusi Valdimir Putin anaonekana kuuchochea zaidi mzozo huo kwa kutia saini amri inayotambua hati za usafiri zinazotolewa na waasi wanaodhibizi majimbo ya Lgansk na Donetsk akisema raia wa Ukraine na watu wasio na uraia wanaoishi katika maeneo hayo sasa wataruhusiwa kuingia na kutoka Urusi bila ya visa.
Urusi imeitaja hatua hiyo kama ya muda hadi pale sulushisho la kisiasa litakapopatikana kurejesha amani katika eneo hilo. Lakini Rais wa Ukraine Petro Poroshenko ameishutumu hatua hiyo ya Urusi na kuitaja thibitisho kuwa Urusi inakiuka sheria za kimataifa na kutaka kuikalia kimabavu Ukraine.
Utawala mpya wa Marekani wa Rais Donald Trump umesema vikwazo vyovyote vilivyowekewa Urusi kutokana na kuichukua rasi ya Crimea kutoka kwa Ukraine na kudaiwa kuuchochea mzozo wa mashariki mwa Ukraine havitaondolewa hadi hatua zipigwe za kutekeleza makubaliano ya kuukomesha mzozo huo.
Mwandishi: Caro Robi/Afp/Reuters
Mhariri: Isaac Gamba