1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano ya kutodukuana kati ya Marekani na Ujerumani yajikokota

16 Januari 2014

Mazungumzo kuhusu kufikiwa makubaliano kati ya Marekani na Ujerumani ya kusitisha udukuzi yanaonekana kukwama huku wabunge wa upinzani nchini Ujerumani wakiishutumu serikali kwa jinsi inavyoshughulikia mzozo huo.

https://p.dw.com/p/1ArUt
Picha: picture-alliance/dpa

Ujerumani imekuwa ikifanya mikutano ya faragha na Umoja wa Ulaya kwa miezi kadhaa sasa ili kufikiwa kwa mkataba wa pamoja na nchi wanachama wa umoja huo wa Ulaya wa kutodukuana, kampeini inayopingwa na Uingereza.

Gazeti la Süddeutsche Zeitung hapo jana liliripoti kuwa mazungumzo kati ya Marekani na Ujerumani kuhusu suala hilo nyeti la udukuzi yako karibu kukwama. Maafisa wa serikali zote mbili wamekanusha vikali ripoti za gazeti hilo.

Je ni kashfa juu ya kashfa?

Misururu hii ya mikuatano ni kufuatia ufichuzi uliofanywa na aliyekuwa mfanyikazi wa shirika la usalama wa kitaifa la Marekani, NSA, Edward Snowden, kuwa shirika hilo limekuwa likidukua mawasiliano ya mamilioni ya watu kote duniani wakiwemo viongozi wa nchi.

Raia wakiandamana kupinga udukuzi wa Marekani
Raia wakiandamana kupinga udukuzi wa MarekaniPicha: picture-alliance/dpa

Ujerumani ilighadhabishwa mno ilivyobainika kuwa mawasiliano ya Kansela wake Angela Merkel ya simu yake ya mkononi pia yalidukuliwa na NSA na kuibua mzozo kati ya nchi hizo mbili ambao ni washirika wa karibu wa muda mrefu.

Taarifa za baadhi ya vyombo vya habari zinaarifu kuwa kumekuwa na mazungumzo ya faragha yanayoongozwa na Ujerumani kuzihimiza nchi za umoja wa Ulaya kukubali kutia saini mkataba wa maelewano wa kutodukuana katika masuala ya kisiasa na kiuchumi.

Iwapo makubaliano hayo yataafikiwa, yataruhusu tu udukuzi katika masuala kama kukabiliana na ugaidi na uingizaji haramu wa silaha za maangamizi makubwa.

Merkel ataka umoja wa Ulaya kushirikiana

Shirika la ujasusi la Ujerumani, Bundesnachrichtedienst, limesema linaongoza mazungumzo hayo kufuatia ombi la kansela Merkel anayetaka kuwe na viwango sawa vya kijasusi katika Umoja wa Ulaya.

Mazungumzo kati ya Marekani na Ujerumani ya kutaka kuafikiana kutodukuana yalianza mwezi Agosti mwaka jana lakini gazeti la New York Times wiki hii limeripoti kuwa huenda Ujerumani isifanikiwe kuishawishi Marekani kuingia katika makubaliano hayo kwani kwa kufanya hivyo ni kuanzisha hali ambayo nchi nyingine pia zitataka kufuata mkondo wa kuishurutisha Marekani kutoidukua.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Reuters

Kiongozi wa chama cha Social Democratic, SPD, bungeni, Thomas Opperman, ameishutumu Marekani kwa kutoonyesha nia ya kuafikiana na Ujerumani.

Na kama kuuchochea moto zaidi mzozo huo wa udukuzi, ni ufichuzi wa hapo jana wa gazeti la New York Times kuwa shirika la usalama wa kitaifa laf Marekani, NSA, limeanzisha mfumo wa kudukua mamilioni ya kompyuta ulimwenguni ambazo hata hazina intaneti kwa kutumia teknoljia ya mawimbi ya redio inayoweza kusambazwa kwa fyuzi ndogo.

Teknolojia hiyo hasa inalenga jeshi la China, Urusi na makundi yanayohusika katika biashara ya dawa za kulevya ya Mexico. NSA pia inadaiwa imeingilia asasi za kibiashara za Umoja wa Ulaya.

Rais wa Marekani, Barack Obama, antarajiwa kutangaza mabadiliko muhimu kuhusu shughuli za shirika hilo la kitaifa la usalama hapo kesho kutokana na mapendekezo ya jopo lililobuniwa kuchunguza shughuli za NSA.

Mwandishi:Caro Robi/afp/Dw English

Mhariri: Josephat Charo