"Tunawindwa kama wanyama"
4 Machi 2015Watu wenye ulemavu wa ngozi ama albino wanaishi kwa wasiwasi nchini Malawi. Wanahofia kuuliwa na viungo vyao kutumika na watu wanaoamini kuwa watajipatia utajiri au madaraka. Kwa mujibu wa chama cha albino nchini Malawi mwaka huu albino watatu wameuliwa kikatili nchini humo. "Tunawindwa kama wanyama," anaeleza msemaji wa chama hicho kinachotetea haki za albino wapatao 10,000 wanaoishi Malawi. Mwanamke mmoja alikutwa amekufa, kichwa chake, miguu na mikono ikiwa imekatwa. Mbali na kufanya upelelezi kuhusu visa vya mauaji, polisi inawatafuta albino wengine ambao hawajulikani walipo.
Inaaminika kwamba viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi vinakwenda kuuzwa nchi jirani ya Tanzania. Huko, serikali ilipiga marufuku shughuli za waganga wa kienyeji kwani wao ndio wanasadikiwa kuwaagiza wateja wao wawaletee viongo vya albino. Tangu mwaka 2000 albino wapatao 70 wameuliwa nchini Tanzania. Polisi inaripoti kuwa jijini Dar es Salaam viungo vya albino mmoja vinafikia bei ya hadi dola za Kimarekani 75,000 ambazo ni sawa na karibu shilingi milioni 140 za Kitanzania.
Watu wa kipekee
Wanaharakati wanasema baada ya serikali ya Tanzania kuanzisha kampeni ya kudhibiti mauaji ya albino, wahalifu sasa wamehamia Malawi. Wazazi wa watoto wenye ulemavu wanaeleza kuogopa hata kuwaruhusu watoto wao waende shule kwani hawajui kama watarudi salama au kama watatekwa.
Albino wako hatarini kwenye nchi nyingi za Kiafrika, zikiwemo Kenya, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Senegal. Shirika la kimataifa la "Under The Same Sun" linalotetea haki za watu hao linaripoti kuuliwa kwa albino 140 katika nchi 25 za Kiafrika. Wengine 219 walikatwa viongo lakini wakaachwa hao.
Imani kwamba Albino ana nguvu za miujiza inatokana na kwamba wengi hushangaa inakuaje wazazi wawili wenye ngozi nyeusi wazae mtoto mwenye ngozi nyeupe, hivyo wanadhani huyo lazima atakuwa na nguvu za kipekee. Jamii nyingine zinachukulia kuzaliwa kwa albino kama laana ya mababu na hivyo akizaliwa mtoto mwenye ulemavu wa ngozi anauliwa. Kwa upande mwingine, watu wa kabila la Yoruba nchini Nigeria na Benin wanaamini kuwa malabino ni watu wa kipekee wanaolindwa na mungu anayeitwa Obatala na kwamba Mungu huyo anapenda rangi nyeupe ndio maana akawapa albino ngozi nyeupe.
Mwandishi: Elizabeth/dpa
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman