1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mamilioni ya Wajerumani Mashariki wahamia Magharibi

30 Oktoba 2019

Tangu wakati wa iliyokuwa Jamhuri ya Ujerumani Mashariki GDR mamilioni ya watu walilihama eneo la Mashariki na kuchochea mgogoro wa kijamii katika eneo hilo. Watu wa Mashariki waliondoka kwa wingi na kuhamia Magharibi.

https://p.dw.com/p/3SDMT
Filmkulisse "Liebe Mauer" von Peter Timm
Picha: picture-alliance/akg-images /Schuetze /Rodemann

Tangu wakati ilipokuwepo iliyokuwa Jamhuri ya Ujerumani Mashariki DDR mamilioni ya watu walilihama eneo la Mashariki na kuchochea mgogoro wa kijamii katika eneo hilo.Wimbi la watu kuondoka kwa wingi upande wa Mashariki liligawika kwa sehemu kubwa tatu.

Katika awamu ya kwanza wimbi hilo lilishuhudiwa baada ya kuundwa kwa dola hilo mwaka 1949 mpaka kipindi ulipojengwa ukuta mwaka 1961 kiasi watu milioni 2.7 waliikimbia Mashariki. Na katika mwaka 1953 pekee raia 331.000 wa iliyokuwa Jamhuri ya Ujerumani Mashariki waliikimbia nchi yao baada ya kuzimwa kwa vuguvugu lililopata umaarufu na kusababisha kutokea umwagikaji mkubwa wa damu.

Awamu ya pili ya watu kuondoka kwa wingi mkubwa Ujerumani Mashariki ilishuhudiwa mwaka 1989 baada ya kuangushwa ukuta wa Berlin. Na kwa hakika baada ya Ujerumani mbili Mashariki na Magharibi kuungana kiasi watu milioni 3.7 waliitupa mkono Ujerumani Mashariki.

Hii ni kusema kwamba kiasi robo ya idadi jumla ya watu wa Ujerumani Mashariki waliikimbia nchi yao. Lakini wimbi hilo halikuishia hapo.Awamu ya tatu ya wimbi hilo imeshuhudiwa mwaka 2000.

Berlin Tag der Deutschen Einheit
Picha: Getty Images/A. Koerner

Watu hao waliokimbia kutoka Mashariki sio tu walikuwa hawajaridhishwa na hali ya kisiasa lakini pia hali ya maendeleo ya kiuchumi haikuwapa hamasa ya kubakia Mashariki,hasa kutoka na kuwepo hali ya wakulima kulazimishwa na mamlaka kulima kwa pamoja na kufanya kilimo kinachoamrishwa na serikali.

Wengi kutoka Mashariki kwahivyo walihisi kuna matumani ya hali kuwa bora zaidi katika ajira upande wa Magharibi. Lakini ukweli ni kwamba sio tu idadi kubwa ya wakimbizi kutoka Ujerumani  Mashariki iliyokuwa tatizo lakini hata mchanganyiko wa kijamii lilikuwa ni suala gumu kwa serikali na jamii kwa Ujumla wake.

Ujerumani Mashariki ilipoteza  vijana wengi waliokimbilia Mashariki,wasomi wakiwemo wataalamu kama vile madaktari na Wahandisi,wote hawa waliikimbia nchi yao Nusu ya wakimbizi hao kutoka Ujerumani Mashariki walikuwa ni vijana chini ya umri wa miaka 25.

Na kufikia miaka ya 1950 GDR ilikuwa imeshapoteza kiasi thuluthi moja ya wasomi wake. Hata hivyo kwa upande wa Jamhuri ya shirikisho ya Ujerumani Magharibi wakimbizi hao kutoka Mashariki walikaribishwa kwa mikono miwili kwasababu kama wanavyosema waswahili mwenyeji njoo mgeni apone.

Berlin Tag der Deutschen Einheit
Picha: Getty Images/A. Koerner

Kwa Magharibi hiki kilikuwa ni kipindi cha mwanzo wa kuufungua ukurasa wa maajabu ya kiuchumi. Takriban kila mahala walikuwa wakitafutwa watu wenye ujuzi wa kufanya kazi za kitalaamu. Kiu kilikuwa kikubwa mno.Na kwa maana hiyo haikuwa vigumu kuwajumuisha katika maisha ya kawaida wakimbizi kutoka Mashariki na wala haikuhitajika gharama kubwa,iwe ni ya kutowa mafunzo au elimi,kila kitu kilikuwa rahisi kabisa.

Kwahivyo wakati Ujerumani Magharibi ikiwa inafaidika kwa kiasi kikubwa kutokana na wasomi na wataalamu wenye ujuzi waliokimbia kutoka Mashariki, GDR au Jamhuri ya Ujerumani Mashariki ilikuwa ikikabiliwa na hali ngumu na mporomoko,iliyosababishwa na kukosekana wataalamu mbali mbali,idadi ndogo ya nguvu kazi pamoja na watu kuendelea kuwa wazee. Ni kutokana na ukweli huo Agosti mwaka 1961 GDR ilifikia uamuzi wa kuifunga mipaka yake ili kuwazuia raia wake kutopata nafasi ya kuhama.

Mwandishi: Freund Alexander

Tafsiri: Saumu Mwasimba

Mhariri: Grace Patricia Kabogo

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW