1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mandela afariki dunia

Abdu Said Mtullya6 Desemba 2013

Babu Madiba, aliekuwa nguzo katika harakati za kupambana na utawala wa kibaguzi nchini Afrika Kusini na rais wa kwanza mwafrika wa taifa hilo ameiaga dunia akiwa na umri wa miaka 95.

https://p.dw.com/p/1ATx6
Mzee Nelson Mandela
Mzee Nelson MandelaPicha: Reuters

Baada ya kuzaliwa, Mandela alipewa jina la Rolihlahla na baba yake Gadla mnamo mwaka wa 1918. Lakini mzee Gadla hakujua kwamba jina hilo lingemletea mwanawe heshima kubwa.

Katika lugha ya Xhosa, Rolihlahla maana ni yule anaeyakwanyua matawi . Pia maana yake ni mtu anaeweza kukorofisha. Na hakika aliukorofisha utawala wa kibaguzi.(kulingana na maana ya jina lake, kama jinsi alivyokuwa anaitwa kwa moyo wa upendo na watu wa Afrika kusini wa rangi zote.)

Bildergalerie Jürgen Schadeberg
Mandela enzi za ujana wake.Picha: J. Schadeberg

Utawala wa makaburu haukusubiri: ulichukua hatua za kulipiza kisasi- Makaburu walimfunga jela Madiba kwa muda wa miaka 27. Aliyoyasema Mandela wakati wa ya Rivonia mnamo mwaka wa 1964 hayatasahaulika. Alisema mahakamani wakati wa kesi hiyo" nipo tayari kuyatoa maisha yangu" Aliyasema hayo katika tamko la kujitetea kwa muda wa saa nne. Mandela alikabiliwa na mashtaka 150 ya vitendo vya hujuma. Alipewa adhabu ya kifungo cha maisha jela.

Wakati alipokuwa kijana ,tayari alishayakwanyua matawi. Baada ya maisha mazuri kama mtoto wa chifu katika jimbo la Transkei, Mandela alionekana kuwa ni kiongozi wa kikundi cha wanafunzi waliokuwa wanafanya upinzani kwenye chuo kikuu. Mandela aliung'oa mzizi wa ndoa alipokuwa kijana.

Alitoroka nyumbani kukwepa ndoa ya kulazimishwa kwa kukimbilia katika jiji la Johannesburg. Muda mfupi baada ya kuwasili katika jiji hilo Mandela aliingiwa moyo wa siasa. Alijiunga na chama cha ANC mnamo mwaka wa 1944. Miaka minne baadaye chama cha makaburu "Nationalist Party" kiliingia madarakani na kuanzisha mara moja mfumo wa ubaguzi wa rangi.

Mnamo mwaka wa 1952 Mandela alifungua ofisi ya uwakili mjini Johannesburg - ya kwanza ya Mwafrika. Katika nyakati hizo kampeni za upinzani za waafrika, dhidi ya utawala wa makaburu zilipamba moto. Kampeni za kutoitii serikali Zilizoongozwa na chama cha ANC

Nelson Mandela tot
Mandela akifurahia jambo wakati w auhai wake.Picha: Reuters

Mandela alitoa mchango mkubwa katika kampeni hizo. Baada ya chama cha ANC kupigwa marufuku mnamo mwaka wa 1961, Mandela aliekuwa bondia wa ridhaa alizindua tawi la kijeshi ili kuanzisha mapambano ya mtutu wa bunduki dhidi ya utawala wa kibaguzi. Na yeye mwenyewe alikuwa kamanda wa tawi hilo,"Umkhonto we Sizwe" mkuki wa taifa. Mandela alisema wakati huo. "Nilitoa tamko ,kutoa mwito wa kuendesha mapambano ya mtutu wa bunduki, kwa sababu serikali haikutuachia njia nyingine."

Alianzisha kampeni ya kuzishambulia taasisi za serikali kwa mtindo wa kujificha. Mandela alisema wakati huo kwamba alianzisha mapambano ya mtutu wa bunduki kwa sababu serikali ya makaburu haikuwapa Waafrika njia nyingine.

Mnamo mwaka wa 1962 Mandela alitoroka na kwenda nje ya Afrika Kusini kwa lengo la kuwatafuta wafadhili na kutafuta mafunzo kwa ajili ya makada wa chama cha ANC. Aliporejea nchini Afrika Kusini, alikamatwa na makaburu. Na baadaye alihukumiwa kifungo katika kesi maaruf ya Rivonia. Aliitumikia miaka 17 katika jela ya kisiwa cha Robben.

Kutokana na kazi ya kuvunja mawe, katika jua kali macho yake yaliathirika sana. Ndiyo sababu ni marufuku kwa wapiga picha kutumia vimweru wakati wa kumpiga picha Mandela .Lakini wakati akiwa jela alianzisha chuo cha masomo-kilichoitwa Chuo Kikuu cha Kisiwa cha Robben. Aliwafundisha wafungwa wenzake kusoma na kuandika.

Leo kizimba namba tano ni miongoni mwa vivutio vikubwa vya utalii nchini Afrika Kusini. Lakini dalili za kuachiwa zilianza kuonekana mnamo mwaka 1988. Lakini miaka mitatu kabla ya hapo aliukataa msamaha ulioambatanishwa na masharti ya kuachana na harakati za mtutu wa bunduki.

Nelson Mandela tot
Nelson MandelaPicha: Picture-Alliance/Photoshot

Lakini mazungumzo ya siri yalifanyika baina yake na wawakilishi wa serikali ya kibaguzi. Mnamo mwaka wa 1990 yalifikiwa mapatano. Na aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini wakati huo Frederik de Klerk alitangaza bungeni kwamba Mandela ameachiwa. Alisema "Nelson Mandela amefunguliwa."

Mnamo mwaka wa 1994 Mandela alikuwa Rais wa kwanza mwafrika nchini Afrika kusini. Tarehe 11 mwezi Februari akiwa ameshikana mikono na mkewe wa hapo awali Winnie Mandela, Madiba alitoka jela baada ya miaka 27 jela. Alitoa mwito:

"Nimepigana dhidi ya ukandamizaji wa watu weupe. Nimepigana dhidi ya ukandamizaji wa watu weusi. Nimeliweka moyoni lengo la jamii huru na ya kidemokrasia ambamo watu wote wataishi pamoja kwa amani na haki sawa. Naishi kwa ajili ya lengo hilo na natumai kulipigania na kulifikia. Lakini iwapo itakuwa lazima, nipo tayari kufa kwa ajili ya lengo hilo."

Madiba alijitoa kwenye mikiki ya siasa mnamo mwaka wa 1999. Kifo cha Mandela kimeacha pengo kubwa . Dunia imempoteza mpigania uhuru na kiongozi adhimu.

Mwandishi:Schadomsky Ludger
Tafsiri:Mtullya Abdu.
Mhariri: Yusuf Saumu